Kutoka 22

Kutoka 22

Sheria za malipizo

1Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.[#2 Sam 12:6; Lk 19:8; Mit 6:31]

2Mwizi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake.[#Kut 20:15; Law 19:11; Kum 5:19; Mt 6:19; 24:43; Lk 18:20; Rum 13:9; Efe 4:28; 1 Pet 4:15; Hes 35:27]

3Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wizi wake.[#Kut 21:2; Mt 18:25]

4Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng'ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili.[#Kut 21:16; Mit 6:31]

5Mtu akilisha mifugo kama shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake.

6Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa.

7Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwizi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili.

8Mwizi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe.

9Kila jambo la kukosana, kama ni la ng'ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu chochote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili.[#Kum 25:1; 2 Nya 19:10]

10Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng'ombe, au kondoo, au mnyama yeyote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa mtu asione;

11patakuwa na kiapo cha BWANA katikati ya watu hao wawili, kwamba alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala hatalipa.[#Ebr 6:16]

12Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, sharti amlipe yule mwenyewe.[#Mwa 31:39]

13Kama aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa.

14Mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama, au akafa, mwenyewe asipokuwapo, lazima atalipa.

15Kama huyo mwenyewe alikuwapo pamoja na mnyama wake, hatalipa; kama ni mnyama wa kukodisha ni gharama ya kukodisha tu atakayepewa mwenyewe.

Sheria za jamii na kidini

16Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe.[#Kum 22:28-29]

17Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo.[#1 Sam 18:25]

18Usimwache mwanamke mchawi kuishi.[#Kum 18:10-11]

19Mtu yeyote alalaye na mnyama sharti atauawa.[#Law 18:23; 20:15-16; Kum 27:21]

20Mtu atakayemchinjia sadaka mungu yeyote, isipokuwa ni yeye BWANA peke yake, na angamizwe kabisa.[#Kum 13:1; 17:2-7; Hes 25:2; Hos 8:14; 1 Fal 18:40]

21Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.[#Kut 23:9; Law 19:33-34; 25:35; Kum 10:19; Zek 7:10; Mal 3:5; Kum 24:17-18; 27:19]

22Usimtese mjane yeyote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima.[#Isa 1:17; Eze 22:7; Kum 10:18]

23Ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao,[#Kum 15:9; Ayu 35:9; 34:28; Yak 5:4]

24na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.[#Ayu 31:23; Zab 109:9]

25Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida.[#Law 25:35-38; Kum 15:7-11; 23:19-20; Neh 5:7; Eze 18:8]

26Ikiwa wewe kwa njia yoyote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa;[#Kum 24:10-13; Ayu 24:3; Mit 20:16; Amo 2:8]

27maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema.

28Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako.[#Mdo 23:5; Mhu 10:20; 2 Pet 2:10]

29Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao wanaume utanipa mimi.[#Mit 3:9]

30Nawe utafanya vivyo hivyo katika ng'ombe wako, na kondoo wako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi.[#Kum 15:19; Law 22:27]

31Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yoyote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.[#Law 17:15; 19:2; Eze 4:14]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya