Kutoka 25

Kutoka 25

Matoleo kwa ajili ya Hema Takatifu

1BWANA akanena na Musa, akamwambia,[#1 Nya 29:3; 2 Kor 9:7]

2Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu.[#1 Nya 29:3; 2 Kor 9:7]

3Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, fedha na shaba,

4na nyuzi rangi za buluu, zambarau na nyekundu, na nguo za kitani safi, na singa za mbuzi;

5na ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na miti ya mjohoro,[#25:5 Katika Kiebrania maana si dhahiri.]

6na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri;

7na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani.[#Kut 28:15]

8Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao.[#Law 4:6; Ebr 3:6; Ufu 21:3]

9Sawasawa na haya yote nikuoneshayo, mfano wa maskani, na mfano wa samani zake zote, ndivyo mtakavyovifanya.

Sanduku la Agano

10Nao na wafanye sanduku la mti wa mjohoro; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu.[#Kut 37:1; Kum 10:3; Ebr 9:4; #25:10 Ni urefu wa kutoka kiwiko cha mkono hadi ncha ya kidole kirefu.]

11Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote.

12Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili.

13Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu.

14Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku.

15Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.[#1 Fal 8:8]

16Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa.[#Kut 16:34; 31:18; 40:20; Kum 10:2; 31:26; 1 Fal 8:9; 2 Fal 11:12]

17Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu.[#Ebr 9:5; Kut 37:6; Rum 3:25; #25:17 Agano au ‘kifuniko’.]

18Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku.

19Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi yawe kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.

20Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema.[#1 Fal 8:7; 1 Nya 28:18]

21Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku.[#Kut 26:34; 40:20]

22Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.[#Kut 29:42; 30:6,36; Law 16:2; Hes 17:4; Eze 9:3; Yak 2:13; 1 Sam 4:4; 6:2; 2 Fal 19:15; Zab 80:1; 90:1; Isa 37:16]

Meza ya mikate iliyowekwa mbele ya Mungu

23Nawe fanya meza ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu.[#Kut 37:10; 1 Fal 7:48; 2 Nya 4:8; Ebr 9:2]

24Uifunike dhahabu safi, na kuifanyia ukingo wa dhahabu wa kuizunguka pande zote.

25Kisha ifanyie upapi wa kuizunguka pande zote, upana wake utakuwa nyanda nne, nawe uufanyie ule upapi ukingo wa urembo wa dhahabu wa kuuzunguka pande zote.

26Uifanyie vikuku vinne vya dhahabu, na kuvitia vile vikuku katika pembe zake nne, katika miguu yake minne.

27Vile vikuku na viwe karibu na ule upapi, ili viwe mahali pa kutilia ile miti, ya kuichukulia meza.

28Fanya ile miti ya mti wa mshita, na kuifunika dhahabu, kwamba ile meza ichukuliwe kwayo.

29Nawe fanya sahani zake, na miiko yake, na makopo yake, na vikombe vyake vya kumiminia; vifanye vyote vya dhahabu safi.[#Kut 37:16; Hes 4:7]

30Nawe utaiweka mikate ya wonyesho juu ya meza mbele yangu daima.[#Law 24:5-8]

Kinara cha taa

31Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, kitako chake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho;[#Kut 37:17; 1 Fal 7:49; Zek 4:2; Ebr 9:2; Ufu 1:12; 4:5]

32nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili[#Hes 8:4; Kut 37:18,19]

33vikombe vitatu vilivyotengenezwa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara;

34na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake;

35na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara.

36Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi.

37Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake.[#Ufu 1:12; Kut 27:21; 30:8; Law 24:3,4; 2 Nya 13:11; Hes 8:2]

38Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi.

39Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote.

40Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, uliooneshwa mlimani.[#Mdo 7:44; Ebr 8:5; Kut 26:30; Hes 8:4; 1 Nya 28:11,19]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya