The chat will start when you send the first message.
1BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonesha;[#Mdo 7:2-3; Ebr 11:8; Mwa 15:7]
2nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;[#Mwa 17:6; 18:18; 46:3; Hes 23:10; Kum 26:5; 1 Fal 3:8]
3nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.[#Gal 3:8; Mwa 24:35; 27:29; Kut 23:22; Hes 24:9; Mwa 22:18; 26:4; 28:14; Zab 72:17; Mdo 3:25]
4Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.
5Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.[#Mwa 11:31; Ebr 11:8]
6Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.[#Yn 4:5; Kum 11:30; Amu 7:1]
7BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye akamjengea BWANA madhabahu huko alikomtokea.[#Mdo 7:5; Gal 3:16; Mwa 17:1; Kum 34:4; Zab 105:9-12; Mwa 13:4]
8Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; Betheli ilikuwa upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea BWANA madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA.
9Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini.[#Mwa 13:3]
10Basi kulikuwa na njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa kali katika nchi.[#Mwa 26:1; Zab 105:13; Mwa 43:1]
11Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso;[#Mwa 26:7]
12basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai.[#Mwa 20:11]
13Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.[#Mwa 20:2; 26:7; Zab 25:21; Efe 4:25]
14Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana.
15Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akapelekwa nyumbani mwa Farao.[#Est 2:16]
16Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng'ombe, na punda dume, na watumwa, na wajakazi, na punda majike, na ngamia.
17Lakini BWANA akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu.[#Mwa 20:18; 1 Nya 16:21; Zab 105:14; Ebr 13:4]
18Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, Ni nini hili ulilonitenda? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo?[#Mwa 20:9; 26:10; Mit 21:1]
19Mbona ulisema, Huyo ni dada yangu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako.
20Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.