Mwanzo 16

Mwanzo 16

Kuzaliwa kwa Ishmaeli

1Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri.[#Amu 13:2; Lk 1:7; Gal 4:24]

2Sarai akamwambia Abramu, kwa kuwa BWANA amenifunga tumbo nisizae, sasa mwingilie mjakazi wangu, labda nitapata uzao kutoka kwake. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai.[#Mwa 30:2]

3Kwa hiyo, baada ya Abramu kukaa miaka kumi katika nchi ya Kanaani, Sarai mkewe Abramu alimtwaa Hajiri Mmisri, mjakazi wake, akampa Abramu mumewe, kama mke.

4Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bimkubwa alikuwa duni machoni pake.[#Mit 30:23]

5Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe.[#Kut 5:21]

6Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mikononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.

7Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri.[#Mwa 25:18]

8Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, na unakwenda wapi? Akanena, Namkimbia bimkubwa wangu Sarai.

9Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bimkubwa wako, ukanyenyekee chini ya mikono yake.[#Efe 6:5-9]

10Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi.[#Mwa 22:15-18; Mal 3:1; Mwa 25:12]

11Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako.[#Kut 2:23,24]

12Naye atakuwa kama punda mwitu kati ya watu, mkono wake utapingana na watu wote na mkono wa kila mtu ukipingana naye; na ataishi kwa ugomvi na jamaa yake yote.[#Mwa 25:18]

13Akampa jina BWANA aliyesema naye, “Wewe U Mungu uonaye,” kwani alisema, “Kweli nimemwona Mungu na nikaendelea kuishi baada ya kumuona?”[#Zab 139:1-12; #16:13 Maana katika Kiebrania si dhahiri.]

14Kwa hiyo kisima kile kiliitwa Beer-lahai-roi. Tazama, kiko kati ya Kadeshi na Beredi.[#16:14 maana yake ni Kisima cha Aliye hai anionaye.]

15Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume; Abramu akamwita jina lake Ishmaeli, yule mwanawe, ambaye Hajiri alimzaa.[#Gal 4:22]

16Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajiri alipomzalia Abramu Ishmaeli.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya