Mwanzo 27

Mwanzo 27

Isaka ambariki Yakobo

1Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa.[#Mwa 48:10; 1 Sam 3:2; Mhu 12:3]

2Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu.[#Mit 27:1; Yak 4:14]

3Basi, nakuomba, chukua uta wako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo;[#Mwa 25:27,28]

4ukaniandalie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa.[#Mwa 48:9,15; 49:28; Kum 33:1; Ebr 11:20]

5Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda mbugani awinde mawindo, ayalete.

6Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena,

7Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu.

8Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza.[#Mwa 27:13]

9Nenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo.

10Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake.[#Mwa 48:15]

11Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini.[#Mwa 25:25]

12Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si baraka.[#Mwa 27:22; 9:25; Kum 27:18]

13Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, nenda ukaniletee wana-mbuzi.[#Mwa 43:9; 1 Sam 25:24; 2 Sam 14:9; Mt 27:25]

14Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye.[#Mwa 27:4,9]

15Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo.[#Mwa 27:27]

16Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake.

17Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate aliouandaa.

18Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu?

19Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Inuka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki.[#1 Fal 13:18; 14:2; Isa 28:15; Zek 13:4]

20Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha.[#Kut 20:7]

21Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo.[#Mwa 27:12]

22Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.

23Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki.[#Mwa 27:16]

24Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi.[#Rum 3:7,8; Efe 4:25]

25Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogezea karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa.

26Isaka, baba yake, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu.

27Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema,[#Hos 14:6; Wim 2:13; Ebr 6:7]

Tazama, harufu ya mwanangu

Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana.

28Mungu na akupe ya umande wa mbingu,[#Ebr 11:20; Kum 33:13,28; 2 Sam 1:21; Hes 18:12; Zab 65:9; Zek 9:17]

Na manono ya nchi,

Na wingi wa nafaka na mvinyo.

29Mataifa na wakutumikie[#Mwa 9:25; 12:3; 49:8; Hes 24:9]

Na makabila wakusujudie,

Uwe bwana wa ndugu zako,

Na wana wa mama yako na wakusujudie.

Alaaniwe yeyote yule atakayekulaani,

Na abarikiwe yeyote yule atakayekubariki.

Esau aomba baraka

30Ikawa Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, na punde tu baada ya Yakobo kutoka mbele ya Isaka, babake, mara Esau ndugu yake akaja kutoka katika kuwinda kwake.

31Naye pia amefanya chakula kitamu akamletea babaye, akamwambia baba yake. Babangu na ainuke, ale mawindo ya mwanawe, ili uweze kunibariki.[#Mwa 27:4]

32Isaka, baba yake, akamwuliza, U nani wewe? Akasema, Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza.

33Isaka akatetemeka tetemeko kuu sana, akasema, Ni nani basi yule aliyetwaa mawindo akaniletea? Nami nimekwisha kula kabla hujaja wewe, nikambariki; naam, naye atabarikiwa.[#Mwa 28:3,4; Hes 23:20; Efe 1:3; Rum 11:29]

34Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikuu na chenye uchungu mwingi sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu.[#Ebr 12:17]

35Akasema, Nduguyo amekuja kwa hila, akaichukua baraka yako.[#1 The 4:6]

36Akasema, Je! Hakuitwa Yakobo kwa haki, maana amejitia mahali pangu mara mbili hizi? Alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa ameichukua baraka yangu. Akasema, Je! Hukuniwekea na mimi mbaraka?[#Mwa 25:29-34]

37Isaka akajibu, akamwambia Esau, Tazama, nimemfanya awe bwana wako, na ndugu zake wote nimempa kuwa watumishi wake; kwa nafaka na mvinyo nimemtegemeza, nami nikufanyie nini sasa, mwanangu?[#2 Sam 8:14]

38Esau akamwambia babaye, Una mbaraka mmoja tu, babangu? Unibariki mimi, mimi nami, Ee babangu. Esau akapaza sauti yake, akalia.[#Ebr 12:17]

39Isaka, baba yake, akajibu, akamwambia,[#Ebr 11:20]

Angalia, penye manono ya nchi patakuwa makao yako,

Na penye umande wa mbingu unaotoka juu.

40Kwa upanga wako wewe utaishi, nawe utamtumikia nduguyo;[#Mwa 25:23; 36:8; 2 Fal 8:20; 2 Sam 8:14; Oba 1:18-20]

Na itakuwa utakapoponyoka,

Utalivunja kongwa lake katika shingo yako.

Yakobo akwepa ghadhabu ya Esau

41Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ile baraka babaye aliyombariki. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.[#Mwa 37:4; 50:3; Oba 1:10; 1 Yoh 3:12]

42Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akatuma mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zake Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua.[#Zab 64:5]

43Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani;[#Mwa 11:31]

44ukae kwake siku chache, hadi ghadhabu ya ndugu yako iishe;

45hadi ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapotuma watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja?

46Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yatanifaidi nini?[#Mwa 24:3; 26:35; 28:8]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya