The chat will start when you send the first message.
1Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki.[#Hes 23:7; Hos 12:12]
2Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima.
3Makundi yote hukusanyika huko, watu wakabingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake.
4Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, ninyi ni watu wa wapi? Wakasema, Sisi tu wa Harani.
5Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua.
6Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo.[#Mwa 43:27]
7Akasema, Tazama, kungali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha.
8Wakasema, Hatuwezi, Mpaka makundi yote yakusanyike, watu wakabingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo.
9Na alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo wa baba yake, maana aliwachunga.[#Kut 2:16]
10Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulibingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo wa Labani, ndugu wa mamaye.[#Kut 2:17]
11Yakobo akambusu Raheli, akalia kwa sauti.[#Mwa 33:4; 45:14; Rum 16:16; 1 Kor 16:20; 2 Kor 13:12; 1 Pet 5:14]
12Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari.[#Mwa 13:8; 24:28]
13Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote.[#Mwa 24:29]
14Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.[#Mwa 2:23; Amu 9:2; 2 Sam 5:1; 19:12,13]
15Labani akamwambia Yakobo, Kwa sababu wewe ni jamaa yangu, basi, je! Unitumikie bure? Niambie mshahara wako utakuwa nini?
16Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli.
17Naye Lea macho yake yalikuwa malegevu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri wa uso.[#29:17 Maana katika Kiebrania si dhahiri.]
18Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo.[#Mwa 31:41; 2 Sam 3:14]
19Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu.
20Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda.[#Mwa 30:26; Wim 8:7]
21Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake.[#Amu 15:1]
22Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu.[#Amu 14:10; Yn 2:1]
23Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia kwake.
24Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake.
25Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda?
26Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa;
27timiza siku zake saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine.[#Amu 14:12]
28Yakobo akafanya hivi, akatimiza siku zake saba. Naye Labani akampa Raheli, binti yake, kuwa mkewe.[#29:28 Katika Kiebrania hakuna Labani.]
29Labani akampa binti yake Raheli mjakazi wake Bilha, awe mjakazi wake.
30Ndipo Yakobo akaingia kwa Raheli, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine.[#Mwa 30:26; 31:41; Hos 12:12; #29:30 Katika Kiebrania hakuna Yakobo.]
31BWANA akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai.[#Zab 127:3; Mwa 30:1]
32Lea akapata mimba akazaa mwana, akampa jina lake, Reubeni, maana alisema, Kwa kuwa BWANA ameona mateso yangu; sasa mume wangu atanipenda.[#Kut 3:7; 4:31; Kum 26:7; Zab 25:18; 106:44]
33Akapata mimba tena akazaa mwana, akasema, Kwa kuwa BWANA amesikia ya kwamba mimi sikupendwa, amenipa na huyu; akamwita jina lake Simeoni.
34Akapata mimba tena, akazaa mwana, akasema, Basi wakati huu mume wangu ataungana nami, kwa sababu nimemzalia wana watatu. Kwa hiyo akamwita jina lake Lawi.
35Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu BWANA; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa.