Mwanzo 30

Mwanzo 30

1Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea dada yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi.[#Mwa 29:31; 37:11; Ayu 5:2]

2Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba?[#Mwa 16:2; 1 Sam 1:5]

3Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae kwa niaba yangu, nami nipate uzao kwa yeye.[#Mwa 16:2; 50:23; Ayu 3:12]

4Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake.[#Mwa 35:22]

5Naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana.

6Raheli akasema, Mungu amenipa haki yangu, naye amesikia sauti yangu, akanipa mwana. Kwa hiyo akamwita jina lake Dani.[#Zab 35:24; 43:1; Omb 3:59]

7Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili.

8Raheli akasema, Kwa mashindano makuu nimeshindana na dada yangu, nikashinda. Akamwita jina lake Naftali.[#Mt 4:13]

9Lea alipoona ya kuwa ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, akampa Yakobo kuwa mkewe.

10Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana.

11Lea akasema, Bahati njema! Akamwita jina lake Gadi.

12Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili.

13Lea akasema, Ni heri mimi, maana wanawake wataniita heri. Akamwita jina lake Asheri.[#Mit 31:28; Lk 1:48]

14Reubeni akaenda siku za mavuno ya ngano akaona tunguja shambani, akazileta kwa Lea mamaye. Ndipo Raheli akamwambia Lea, Nipe mimi baadhi ya tunguja za mwanao.[#Wim 7:13; Mwa 25:30]

15Naye akamwambia, Je, Ni jambo dogo kuninyang'anya mume wangu; hata wataka kuzitwaa tunguja za mwanangu pia? Raheli akamwambia, Kwa hiyo atalala kwako usiku huu kwa tunguja za mwanao.[#Hes 16:9]

16Yakobo akaja kutoka kondeni jioni, Lea akatoka kumlaki, akasema, Lazima uje kwangu, kwa sababu nimekukodi, kwa tunguja za mwanangu; akalala kwake usiku ule.

17Mungu akamsikia Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano.

18Lea akasema, Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nimempa mume wangu mjakazi wangu. Akamwita jina lake Isakari.

19Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita.

20Lea akasema, Mungu amenipa mahari njema, sasa mume wangu atakaa nami, kwa kuwa nimemzalia wana sita. Akamwita jina lake Zabuloni.

21Baadaye akazaa binti, akamwita jina lake Dina.

22Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo.[#Mwa 8:1; 29:31; 1 Sam 1:19]

23Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu.[#1 Sam 1:6; Isa 4:1; Lk 1:25]

24Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Bwana aniongeze mwana mwingine.[#Mwa 35:17]

Yakobo abarikiwa zaidi ya Labani

25Ikawa Raheli alipomzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, Nipe ruhusa niende kwetu, na kwenye nchi yangu.[#Mwa 18:33; 24:55; 31:55]

26Nipe wake zangu na watoto wangu, niliokutumikia, niende zangu, maana umejua utumishi wangu niliokutumikia.[#Mwa 29:20]

27Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako.[#Mwa 26:24; 39:3,5; Zab 1:3; Isa 61:9]

28Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa.[#Mwa 29:15]

29Akamwambia, Umejua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi wanyama wako walivyokuwa kwangu.[#Mwa 31:6; Mt 24:45; Tit 2:10]

30Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi, BWANA akakubariki kila nilikokwenda. Basi sasa, nitaangalia lini mambo ya nyumba yangu mwenyewe?[#1 Tim 5:8]

31Akamwuliza, Nikupe nini? Yakobo akasema, Usinipe kitu; ukinifanyia neno hili, nitalisha wanyama wako tena na kuwalinda.

32Nitapita katika wanyama wako wote leo, na kutoa huko kila mnyama aliye na madoadoa na marakaraka, na kila mnyama mweusi katika hao kondoo, na aliye na marakaraka na madoadoa katika mbuzi; nao watakuwa mshahara wangu.[#Mwa 31:8]

33Na haki yangu itanishuhudia katika siku zijazo, utakapokuja kwa habari ya mshahara wangu ulioko kwako. Kila asiye madoadoa au marakaraka katika mbuzi, au asiye mweusi katika kondoo, akionekana kwangu, itahesabiwa kuwa ameibiwa.[#Zab 37:6]

34Labani akasema, Tazama, na iwe hivi kama usemavyo.

35Basi akatoa siku ile mbuzi dume walio na milia na madoadoa, na mbuzi wake walio na madoadoa na marakaraka, kila aliye na doa jeupe, na kondoo wote waliokuwa weusi, akawatia mikononi mwa wanawe.

36Akajitenga na Yakobo mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akachunga wanyama wa Labani waliosalia.

37Yakobo akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda, mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito.[#Mwa 31:9]

38Akazisimamisha fito hizo alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa.

39Wanyama wakapata mimba mbele ya hizo fito, wakazaa wanyama walio na milia, na madoadoa, na marakaraka.

40Na Yakobo akawatenga wana-kondoo, akazielekeza nyuso za makundi zielekee wale waliokuwa na milia, na kila aliyekuwa mweusi katika wanyama wa Labani. Akaweka kando wanyama wake mwenyewe, wala hakuwachanganya pamoja na wanyama wa Labani.

41Ikawa kila walipopata mimba wanyama wenye nguvu, Yakobo akaziweka zile fito mbele ya macho ya hao wanyama katika mabirika ili kwamba wachukue mimba kati ya zile fito,

42lakini wanyama walipodhoofika hakuziweka zile fito. Basi wale dhaifu walikuwa wa Labani, na wenye nguvu walikuwa wa Yakobo.

43Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na punda.[#Mwa 28:15; Ayu 1:3; Mhu 2:7; Eze 39:10; Mwa 13:2; 24:35; 26:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya