Mwanzo 34

Mwanzo 34

Dina abakwa

1Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi.[#Mwa 30:21; Tit 2:5]

2Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri.[#Mwa 6:2; Amu 14:1]

3Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri.[#Isa 40:2; Hos 2:14]

4Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu.[#Amu 14:2]

5Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hadi walipokuja.

6Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye.

7Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka malishoni; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, jambo lisilostahili kutendeka.[#Mwa 49:7; 2 Sam 13:12,21; Yos 7:15; Amu 20:6; Kum 23:17]

8Hamori akasema nao, akinena, roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe.

9Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu.[#Kut 23:32]

10Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo.[#Mwa 13:9; 20:15; 42:34; 47:27]

11Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa.

12Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu.[#Kut 22:16; Kum 22:29; 1 Sam 18:25]

13Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, dada yao,[#2 Sam 13:24]

14wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe dada yetu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu.[#Yos 5:9]

15Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu,

16ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja.

17Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa binti yetu, nasi tutakwenda zetu.

18Maneno yao yakawa mema machoni pa Hamori, na machoni pa Shekemu, mwana wa Hamori.

19Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa mwenye heshima kuliko wote nyumbani mwa babaye.[#1 Nya 4:9]

20Hamori, na Shekemu mwanawe, wakaja langoni pa mji wao, wakasema na watu wa mji wao, wakinena,[#2 Sam 15:2; Rut 4:1]

21Watu hawa wana amani nasi, basi na wakae katika nchi, na kufanya biashara humo; kwa maana nchi ni kubwa, yawatosha; na tuwatwae binti zao kuwa wake zetu, na binti zetu tuwape wao.

22Lakini kwa sharti hiyo moja tu watapatana nasi wakae wote kwetu, tuwe watu wamoja, kama tukitahiriwa kila mwanamume, kama wao walivyotahiriwa.

23Je! Kondoo zao, na mali zao, na wanyama wao wote hawatakuwa mali zetu? Basi na tupatane nao tu, nao watakaa kwetu.

24Wakawasikia Hamori na Shekemu mwanawe, wote watokeao katika lango la mji wake. Wakatahiriwa kila mwanamume, wote watokao katika lango la mji wake.[#Mwa 23:10]

Ndugu zake Dina walipiza Kisasi

25Ikawa siku ya tatu, walipokuwa wakiumwa sana, wana wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, nduguze Dina, wakatwaa kila mtu upanga wake, wakaujia mji kwa ujasiri, wakawaua wanaume wote.[#Mwa 49:5-7]

26Wakawaua Hamori, na Shekemu mwanawe, kwa upanga, wakamtwaa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakatoka.

27Wana wa Yakobo wakawajia hao waliouawa, wakaupora mji kwa sababu wamemharibu dada yao.

28Wakachukua kondoo wao, na ng'ombe wao, na punda wao, na vitu vilivyokuwamo mjini, na vile vilivyokuwako kondeni.

29Wakatwaa na mali yao zote, watoto wao wote, na wake zao wakateka na hata wakapora vyote vilivyokuwemo nyumbani.

30Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, Mmenitaabisha, kunifanya ninuke vibaya kati ya watu wa nchi hii, Wakanaani na Waperizi; na mimi, kwa kuwa watu wangu ni haba, watanikusanyikia, na kunipiga, nami nitaangamizwa, mimi na nyumba yangu.[#Mwa 49:6; Yos 7:25; Kut 5:21; 1 Sam 13:4; Kum 4:27; Zab 105:12]

31Nao wakasema, Je! Ni vema amtendee dada yetu kama kahaba?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya