The chat will start when you send the first message.
1Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake.
2Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu.
3Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda wao.
4Na walipotoka mjini, kabla hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema?
5Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwacho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi.
6Akawafuata, akawapata, na kuwaambia maneno hayo.
7Wakamwambia, Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Hasha! Watumwa wako wasifanye hivi.
8Tazama, hizo fedha mlizoziona kinywani mwa magunia yetu tumekuletea tena kutoka nchi ya Kanaani. Tuwezeje sisi kuiba nyumbani mwa Bwana wako fedha au dhahabu?[#Mwa 43:21]
9Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwa watumwa wako, na afe, na sisi nasi tutakuwa watumwa wa bwana wangu.[#Mwa 31:32]
10Akasema, Basi na iwe hivyo kama mlivyosema, Mtu atakayeonekana kuwa nacho atakuwa mtumwa wangu, na ninyi mtakuwa hamna hatia.
11Wakafanya haraka, wakashusha kila mtu gunia lake, na kufungua kila mtu gunia lake.
12Naye akatafuta, akaanza kwa mkubwa na kuisha kwa mdogo. Kikombe kikaonekana katika gunia la Benyamini.
13Wakararua nguo zao, wakaweka kila mtu mzigo wake juu ya punda wake, wakarudi mjini.[#Mwa 37:29,34; Hes 14:6; 2 Sam 1:11]
14Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi.[#Mwa 37:7]
15Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi?
16Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake.[#Ayu 40:4; Mwa 44:9]
17Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi nendeni zenu kwa amani kwa baba yenu.[#Yos 22:29; 1 Sam 12:23; Lk 20:16; Rum 3:4,6; 1 Kor 6:15; Gal 2:17]
18Ndipo Yuda akamkaribia, akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao.[#Mwa 18:30,32; Kut 32:22; Mit 19:12; Mwa 41:40]
19Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu?
20Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda.[#Mwa 37:3]
21Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie.[#Mwa 42:15,20]
22Tukakuambia, bwana wangu, Kijana hawezi kumwacha babaye, maana akimwacha babaye, babaye atakufa.
23Ukatuambia watumwa wako, Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena[#Mwa 43:3,5]
24Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu.
25Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo.[#Mwa 43:2]
26Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka, maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi.
27Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili;[#Mwa 46:19]
28mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo.[#Mwa 37:33]
29Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu kwa msiba kaburini.[#Mwa 42:36,38]
30Basi, nikienda kwa mtumwa wako, baba yangu, na huyu kijana hayupo pamoja nasi, iwapo roho yake imeshikamana na roho ya kijana;[#1 Sam 18:1]
31itakuwa atakapoona ya kwamba huyu kijana hayuko, atakufa; na watumwa wako watashusha mvi za mtumwa wako, baba yetu, kwa huzuni kaburini.
32Kwa maana mtumwa wako alijifanya mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, Nisipomrudisha kwako, nitakuwa na hatia kwa baba yangu daima.[#Mwa 43:9]
33Basi, sasa nakusihi, uniache mimi mtumwa wako nikae badala ya huyu kijana kuwa mtumwa wa bwana wangu; na huyu kijana umwache aende pamoja na nduguze.[#Kut 32:32]
34Kwa maana nitawezaje kumwendea baba yangu, na huyu kijana hayuko pamoja nami? Nisije nikayaona mabaya yatakayompata baba yangu.