The chat will start when you send the first message.
1Sala ya nabii Habakuki.[#3:1 iliyoimbwa kwa Shigionothi.]
2Ee BWANA, nimesikia habari zako, nami naogopa;
Ee BWANA, fufua kazi yako katikati ya miaka;
Katikati ya miaka tangaza habari yake;
Katika ghadhabu kumbuka rehema.
3Mungu alikuja kutoka Temani,
Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani.
Utukufu wake ukazifunika mbingu,
Nayo dunia ikajaa sifa yake.
4Mwangaza wake ulikuwa kama nuru;
Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake;
Ndipo ulipofichwa uweza wake.
5Mbele zake ilikwenda tauni,
Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake.
6Akasimama na kuitikisa dunia;[#Kut 23:31; Kum 32:8; Hes 21:24,34]
Akatazama, mataifa yakatetemeka;
Na milima ya zamani ikatawanyika;
Vilima vya kale vikainama;
Miendo yake ilikuwa kama siku za kale.
7Niliziona hema za Kushani zikitaabika;
Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka.
8Je! BWANA aliikasirikia mito?[#Kut 14:21,22]
Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito,
Au ghadhabu yako juu ya bahari,
Hata ukapanda farasi wako,
Katika magari yako ya wokovu?
9Uta wako ukafanywa wazi kabisa;
Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti;
Ukaipasua nchi kwa mito.
10Milima ilikuona, ikaogopa;
Gharika ya maji ikapita;
Vilindi vikatoa sauti yake,
Vikainua juu mikono yake.
11Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao;
Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa,
Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao.
12Ulikwenda katikati ya nchi kwa ghadhabu;[#Zab 44:2,3; Mik 4:13]
Ukawapura mataifa kwa hasira.
13Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako,[#2 Sam 5:20]
Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako;
Ukakiponda kichwa cha nyumba ya waovu,
Ukiuweka wazi msingi hata mwambani.
14Ukakichoma kichwa cha mashujaa wake kwa fimbo zao wenyewe;
Wakaja kama kisulisuli ili kunitawanya;
Kama wakifurahi kuwameza maskini kwa siri.
15Ukaikanyaga bahari kwa farasi wako,
Chungu ya maji yenye nguvu.
16Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka,
Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile;
Ubovu ukaingia mifupani mwangu,
Nikatetemeka katika mahali pangu;
Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki,
Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu.
17Maana mtini hautachanua maua,[#2 Kor 4:8,9]
Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda;
Taabu ya mzeituni itakuwa bure,
Na mashamba hayatatoa chakula;
Zizini hamtakuwa na kundi,
Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;
18Walakini nitamfurahia BWANA[#Zab 42:5; Isa 61:10]
Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.
19MUNGU, aliye BWANA, ni nguvu zangu,[#2 Sam 22:34; Zab 18:33; 27:1]
Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu,
Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.