The chat will start when you send the first message.
1Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa subira katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,[#Ebr 10:36; Rum 7:21; 1 Kor 9:24]
2tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi katika mkono wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.[#Ebr 2:10; Zab 110:1]
3Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili upinzani mkuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.[#Lk 2:34]
4Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;
5tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana,[#Ayu 5:17; Mit 3:11-12]
Mwanangu, usiyadharau maonyo ya Bwana,
Wala usife moyo ukiadhibiwa naye;
6Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humuonya[#Ufu 3:19]
Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
7Ni kwa ajili ya kuonywa mnastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyeonywa na babaye?
8Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.[#Zab 73:14,15]
9Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawaheshimu; basi si ni afadhali zaidi kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi?[#Hes 16:22]
10Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.
11Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoeshwa nayo matunda ya haki yenye amani.[#2 Kor 4:17,18; Yak 3:17]
12Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza,[#Isa 35:3]
13mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.[#Mit 4:26]
14Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;[#Zab 34:14; Mt 5:8; Rum 12:18; 2 Tim 2:22]
15mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.[#Kum 29:18; Mdo 8:23]
16Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja.[#Mwa 25:29-34]
17Maana mnajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.[#Mwa 27:30-40]
18Maana hamkufikia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingu jeusi, na giza, na tufani,[#Kut 19:12,16-22; 20:18-21; Kum 4:11-12; 5:22-27]
19na mlio wa baragumu na sauti ya maneno; ambayo wale walioisikia walisihi wasiambiwe neno lolote lingine;[#Kut 19:19; 20:19; Kum 5:23]
20maana hawakuweza kustahimili neno lile lililoamriwa, Hata mnyama akiugusa huo mlima atapigwa kwa mawe.[#Kut 19:12-13]
21Na hayo yaliyoonekana jinsi yalivyokuwa ya kutisha, hata Musa akasema, Nimeshikwa na hofu na kutetemeka.[#Kum 9:19]
22Bali ninyi mmeufikia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi,[#Ufu 14:1; 21:2; 5:11; Gal 4:26]
23mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika,[#Lk 10:20]
24na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.[#Mwa 4:10; Ebr 9:15; 11:4; 1 Pet 1:2]
25Angalieni msimkatae yeye anenaye. Maana ikiwa hawakuokoka wale waliomkataa yeye aliyewaonya juu ya nchi, zaidi sana hatutaokoka sisi tukijiepusha na yeye atuonyaye kutoka mbinguni;[#Kut 20:22; Ebr 2:2; 10:28,29]
26ambaye sauti yake iliitetemesha nchi wakati ule; lakini sasa ameahidi akisema, Mara moja tena nitatetemesha si nchi tu, bali na mbingu pia.[#Hag 2:6]
27Lakini neno lile, Mara moja tena, ladhihirisha kuhamishwa vile viwezavyo kutetemeshwa, kama vitu vilivyoumbwa, vitu visivyoweza kutetemeshwa vikae.
28Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza kutetemeshwa, na muwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho;
29maana Mungu wetu ni moto ulao.[#Kum 4:24; 9:3; Isa 33:14]