Isaya 64

Isaya 64

1Laiti ungepasua mbingu, na kushuka, ili milima itetemeke mbele zako;

2kama vile moto uchomapo vichaka, na moto uchemshapo maji; ili kuwajulisha adui zako jina lako, mataifa wakatetemeke mbele zako!

3Ulipofanya mambo ya kutisha tusiyoyatazamia, ulishuka, milima ikatetemeka mbele zako.

4Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye.[#Zab 31:19; Kol 1:26,27; 1 Tim 3:16; Ufu 21:1-4; 1 Kor 2:9,10]

5Wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako; tazama, ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika dhambi kwa muda mrefu, nasi Je! Tutaokolewa?[#Mdo 10:35; Mal 3:6]

6Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.[#Flp 3:9]

7Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.[#Hos 7:7]

8Lakini sasa, Ee BWANA, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.[#Yer 18:6; Efe 2:10]

9Ee BWANA, usione hasira nyingi, wala usiukumbuke uovu siku zote; tazama, angalia, twakusihi, sisi sote tu watu wako.

10Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa, Sayuni umekuwa jangwa, Yerusalemu umekuwa ukiwa.

11Nyumba yetu takatifu, nzuri, walimokusifu baba zetu, imeteketea moto; vitu vyetu vyote vyenye kupendeza vimeharibika.[#2 Fal 25:9; Zab 74:7; Eze 24:21]

12Utajizuia usiyaangalie mambo haya, Ee BWANA? Utanyamaza, na kutuadhibu vikali?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya