The chat will start when you send the first message.
1Ndipo BWANA akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao.[#Kut 32:11-14; Hes 14:13-19; 1 Sam 7:5-9]
2Kisha itakuwa, hapo watakapokuambia, Tutoke, tuende wapi? Utawaambia, BWANA asema hivi, Walioandikiwa kufa, watakwenda kufa; au kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga; au kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa, au kutekwa nyara, watakuwa mateka.[#Zek 11:9; Ufu 13:10]
3Nami nitaamrisha juu yao namna nne, asema BWANA; upanga uue, na mbwa wararue, na ndege wa angani, na wanyama wakali wa nchi, wale na kuangamiza.[#Law 26:16; Kum 28:26]
4Nami nitawafanya kuwa kitu cha kutisha katika falme zote za duniani, kwa sababu ya Manase, mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda, kwa sababu ya mambo aliyoyatenda katika Yerusalemu.[#Eze 23:46; 2 Fal 21:1-16; 2 Nya 33:1-9]
5Maana ni nani atakayekuhurumia, Ee Yerusalemu? Au ni nani atakayekulilia? Au ni nani atakayegeuka upande ili kuuliza habari za hali yako?[#Isa 51:19]
6Umenikataa mimi, asema BWANA, umerudi nyuma; ndiyo maana nimenyosha mkono wangu juu yako, na kukuangamiza; nimechoka kwa kughairi.[#Hos 13:14]
7Nami nimewapepea kwa kipepeo katika malango ya nchi nimewaondolea watoto wao, nimewaharibu watu wangu; hata hivyo hawakurudi na kuziacha njia zao.[#Isa 9:13; Yer 5:3]
8Wajane wao wameongezeka kwangu kuliko mchanga wa bahari; nimeleta mwenye kuteka wakati wa adhuhuri juu ya mama wa vijana; nimeleta uchungu na hofu kuu impate ghafla.
9Mwanamke aliyezaa watoto saba anazimia; ametoa roho; jua lake limekuchwa, ikiwa bado ni wakati wa mchana; ameaibika na kutwezwa; na mabaki yao nitawatoa kwa upanga mbele ya adui zao, asema BWANA.[#1 Sam 2:5; Isa 47:9; Amo 8:9]
10Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani.[#Ayu 3:1]
11BWANA akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu.
12Je! Mtu aweza kuvunja chuma, naam, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13Mali yako na hazina zako nitazitoa kuwa nyara, bila kulipwa thamani yake; naam, kwa sababu ya dhambi zako zote, hata katika mipaka yako yote.[#Zab 44:12; Isa 52:3; Yer 17:3]
14Nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana moto umewashwa katika hasira yangu, utakaowateketeza ninyi.[#Kum 32:22]
15Ee BWANA, unajua wewe; unikumbuke, unijie, ukanilipizie kisasi juu yao wanaoniudhi; usiniondoe kwa uvumilivu wako; ujue ya kuwa ni kwa ajili yako nilivyopatikana na matukano.[#Ayu 10:7; Yn 21:15-17; Zab 17:3; 69:7; Yer 12:3; 11:20; Mt 5:10-12; 1 Pet 4:14-16]
16Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi.[#Eze 3:1; Ayu 23:12]
17Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, niliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu.[#Zab 1:1]
18Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha langu halina dawa, linakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu?[#Yer 30:15; Ayu 6:15]
19Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejesha, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao.[#Zek 3:7; Eze 22:26]
20Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema BWANA.
21Nami nitakuokoa kutoka kwa mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa kutoka kwa mkono wao wenye kutisha.[#Isa 49:25]