The chat will start when you send the first message.
1Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa BWANA, kusema,[#2 Fal 23:36—24:6; 2 Nya 36:5-7]
2BWANA asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya BWANA, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya BWANA; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja.[#Yer 7:2; 19:14; Lk 19:47,48; Yn 8:2; Kut 23:14; Kum 12:5; Mt 28:20; Mdo 20:27]
3Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya matendo yao maovu.[#Yer 36:3; 18:8]
4Nawe utawaambia, BWANA asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu,[#Law 26:14; Kum 28:15]
5kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza;[#Yer 7:13]
6basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa mataifa yote ya dunia.[#1 Sam 4:10; Yos 18:1; Zab 78:60; Isa 65:15; Yer 7:12-14]
7Na makuhani, na manabii, na watu wote, wakamsikia Yeremia, hapo aliposema maneno haya katika nyumba ya BWANA.
8Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote BWANA aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, Bila shaka utakufa.[#Amo 5:10; Mt 27:20]
9Kwa nini umetabiri kwa jina la BWANA, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya BWANA.
10Na wakuu wa Yuda waliposikia habari za mambo haya, wakatoka katika nyumba ya mfalme, wakapanda juu mpaka nyumbani kwa BWANA; wakaketi, hapo watu waingiliapo katika lango jipya la nyumba ya BWANA.[#2 Fal 15:35]
11Ndipo hapo makuhani, na manabii, wakawaambia wakuu na watu wote, wakisema, Mtu huyu anastahili hukumu ya kifo, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu.[#Yer 38:4; Mt 26:61]
12Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, BWANA ndiye aliyenituma kutabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia.
13Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya BWANA, Mungu wenu; naye BWANA atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu.[#Isa 1:19; 55:7; Yer 7:3; 35:15; 36:3; Hos 14:1,2]
14Lakini kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu.[#Yer 38:5]
15Lakini jueni hakika kwamba, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli BWANA amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia.
16Ndipo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani, na manabii, wakisema, Mtu huyu hastahili hukumu ya kifo; kwa maana amesema nasi katika jina la BWANA Mungu wetu.
17Ndipo watu kadhaa miongoni mwa wazee wa nchi wakaondoka, wakanena na mkutano wa watu, wakisema,[#Mdo 5:34]
18Mikaya Mmorashti, alitabiri katika siku za Hezekia, mfalme wa Yuda; akasema na watu wote wa Yuda, ya kwamba, BWANA wa majeshi asema hivi, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu, na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni.[#Mik 1:1; 3:12]
19Je! Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda, walimwua Mikaya? Je! Hakumcha BWANA, na kumwomba BWANA awafadhili; naye BWANA akaghairi, asiyatende mabaya yale aliyoyatamka juu yao? Lakini sisi tuko karibu kujiletea maafa makuu wenyewe.[#2 Nya 32:26; Kut 32:14; 2 Sam 24:16; Mdo 5:39]
20Tena, kulikuwa na mtu aliyetabiri katika jina la BWANA, Uria, mwana wa Shemaya, wa Kiriath-Yearimu; yeye naye alitabiri juu ya mji huu, na juu ya nchi hii, sawasawa na maneno yote ya Yeremia;
21na Yehoyakimu, mfalme, na mashujaa wake wote, na wakuu wake wote, waliposikia maneno yake, mfalme akataka kumwua; lakini Uria alipopata habari, aliogopa, akakimbia akaenda Misri.[#2 Nya 16:10; 24:21; 1 Fal 19:3]
22Basi, mfalme Yehoyakimu akatuma watu waende Misri, Elnathani, mwana wa Akbori, na watu wengine pamoja naye, kwenda Misri;[#Zab 12:8; Mit 29:12]
23wakamtoa Uria katika Misri, wakamleta kwa Yehoyakimu, mfalme; naye akamwua kwa upanga, akamtupa yule maiti katika makaburi ya watu wasio na cheo.[#Mt 23:31]
24Lakini mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani, alikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe.[#2 Fal 22:12-14; Yer 39:14]