Yeremia 33

Yeremia 33

Kuponywa baada ya adhabu

1Tena, neno la BWANA likamjia Yeremia mara ya pili, hapo alipokuwa angali amefungwa katika uwanja wa walinzi, kusema,[#Yer 32:2; 37:21]

2BWANA alitendaye jambo hili, BWANA aliumbaye ili alithibitishe; BWANA ndilo jina lake; asema hivi,[#Isa 37:26]

3Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.[#Mwa 18:17; Kum 4:7,29; Zab 50:15; Isa 55:6,7; Yer 29:12; Mdo 2:21]

4Maana BWANA, Mungu wa Israeli asema hivi, kuhusu nyumba za mji huu, na kuhusu nyumba za wafalme wa Yuda, zilizobomolewa ili kuyapinga maboma na upanga;[#Yer 32:24]

5Wanakuja kupigana na Wakaldayo, lakini ni kuzijaza kwa mizoga ya watu, niliowaua katika hasira yangu na ghadhabu yangu, ambao kwa ajili ya uovu wao wote nimeuficha mji huu uso wangu.

6Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.[#Yer 30:17]

7Nami nitawarudisha wafungwa wa Yuda, na wafungwa wa Israeli, na kuwajenga kama kwanza.[#Yer 32:44; Isa 1:26]

8Nami nitawasafisha uovu wao wote, ambao kwao wamenitenda dhambi; nami nitawasamehe maovu yao yote, ambayo kwayo wamenitenda dhambi, na kukosa juu yangu.[#Zab 85:2,3; Isa 40:2; Yer 31:34; Zek 13:1; Ebr 9:13; Mik 7:18; 1 Yoh 1:7-9]

9Na mji huu utakuwa kwangu jina la furaha, na sifa na utukufu, mbele ya mataifa yote ya dunia, watakaosikia habari ya mema yote niwatendeayo, nao wataogopa na kutetemeka, kwa sababu ya mema yote na amani nitakaoupatia mji huo.[#Ezr 1:2; Isa 62:7; 60:5]

10BWANA asema hivi, katika mahali hapo ambapo mnasema kwamba ni ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, naam, katika miji ya Yuda na katika njia za Yerusalemu, zilizo ukiwa, hazina mwanadamu wala mwenyeji wala mnyama,

11itasikika tena sauti ya furaha na sauti ya shangwe, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi, sauti yao wasemao Mshukuruni BWANA wa majeshi, maana BWANA ni mwema, rehema zake ni za milele; na sauti zao waletao sadaka za shukrani nyumbani kwa BWANA. Kwa kuwa nitawarudisha wafungwa wa nchi hii kama kwanza, asema BWANA.[#1 Nya 16:34; 2 Nya 5:13; 7:3; Ezr 3:11; Zab 100:5; 106:1; 107:1; 118:1; 136:1; Ufu 18:23; Law 7:12; Yon 2:9; Ebr 13:15]

12BWANA wa majeshi asema hivi, Katika mahali hapa, palipo ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, na katika miji yake yote, yatakuwapo makao ya wachungaji wakiwalaza kondoo wao.[#Isa 65:10]

13Katika miji ya nchi ya vilima, katika miji ya nchi tambarare, katika miji ya Negebu, na katika nchi ya Benyamini, na katika mahali palipo karibu na Yerusalemu, na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mikono yake anayewahesabu, asema BWANA.[#Yer 17:26; Law 27:32]

Chipukizi la haki na agano la Daudi

14Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, kuhusu nyumba ya Israeli, na katika habari za nyumba ya Yuda.[#Yer 23:5-6; 29:10]

15Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii.[#Isa 4:2]

16Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA ni haki yetu.[#Kum 33:28; Isa 45:17]

17Maana BWANA asema hivi, Daudi hatakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha nyumba ya Israeli;[#2 Sam 7:12-16; 1 Fal 2:4; 1 Nya 17:11-14]

18wala makuhani Walawi hawatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu, na kutoa sadaka za kuteketezwa, na kufukiza matoleo, na kufanya dhabihu daima.[#Hes 3:5-10; Mal 1:11; Rum 12:1; 1 Pet 2:5,9; Ufu 1:6]

19Neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema,

20BWANA asema hivi, Kama mkiweza kulivunja agano langu la mchana, na agano langu la usiku, hata usiwepo tena mchana na usiku kwa wakati wake,[#Mwa 8:22; Zab 89:37; Isa 54:9; Yer 31:36]

21ndipo agano langu nililolifanya na Daudi, mtumishi wangu, laweza kuvunjika, hata asiwe na mwana wa kumiliki katika kiti chake cha enzi; tena agano langu nililofanya na Walawi makuhani, wahudumu wangu, laweza kuvunjika.

22Kama vile jeshi la mbinguni haliwezi kuhesabiwa, wala mchanga wa bahari kupimwa; ndivyo nitakavyoongeza wazao wa Daudi, mtumishi wangu, na Walawi wanaonihudumia.[#Mwa 13:16; 15:5; Yer 31:37]

23Kisha neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema,

24Je! Hufikiri neno hili walilolisema watu hawa, wakinena, Jamaa zile mbili alizozichagua BWANA amezitupilia mbali? Hivyo ndivyo wanavyowadharau watu wangu, ili wasiwe taifa tena mbele yao.[#Mwa 8:22; Yer 31:35; Zab 74:16; 104:19]

25BWANA asema hivi, Ikiwa agano langu la mchana na usiku sikuliweka imara, ikiwa mimi sikuziamuru kawaida za mbingu na dunia;

26ndipo nitawatupilia mbali wazao wa Yakobo, na Daudi, mtumishi wangu, hata nisitwae wazao wake watawale juu ya wazao wa Abrahamu, na Isaka, na Yakobo; kwa maana nitawarudisha wafungwa wao, nami nitawarehemu.[#Isa 14:1; Yer 31:20; Zek 10:6]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya