Yeremia 34

Yeremia 34

Kufa kwa Sedekia katika uhamisho kwatabiriwa

1Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, hapo Nebukadneza, mfalme wa Babeli, na jeshi lake lote, na falme zote za dunia zilizokuwa chini ya mamlaka yake, na makabila yote ya watu, walipopigana na Yerusalemu, na miji yake yote, kusema,[#2 Fal 25:1-11; 2 Nya 36:17-21; Dan 2:37; Yer 32:2; 1:15]

2BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nenda ukaseme na Sedekia, mfalme wa Yuda, ukamwambie, BWANA asema hivi, Tazama, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto;[#Yer 21:10; 32:29]

3tena wewe hutaokoka mkononi mwake, lakini hakika utakamatwa, na kutiwa katika mikono yake; na utatazamana macho kwa macho na mfalme wa Babeli, naye atasema nawe mdomo kwa mdomo, nawe utakwenda Babeli.[#Yer 32:4]

4Hata hivyo lisikie neno la BWANA, Ee Sedekia, mfalme wa Yuda; BWANA asema hivi kukuhusu; hutakufa kwa upanga;

5utakufa katika amani; na kama walivyofukizia baba zako, wafalme wa zamani waliokutangulia, ndivyo watakavyokufukizia; na kukulilia wakisema, Aa, BWANA! Kwa maana mimi nimelinena neno hili, asema BWANA.[#2 Nya 16:14; Dan 2:46; Yer 22:18]

6Basi Yeremia, nabii, akamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno hayo yote katika Yerusalemu,[#1 Fal 21:19; Eze 2:7; Mt 14:4]

7wakati ule jeshi la Babeli walipopigana na Yerusalemu na miji yote ya Yuda iliyosalia, na Lakishi, na Azeka; kwa maana miji hiyo tu ndiyo iliyosalia katika miji ya Yuda yenye maboma.[#2 Fal 18:13; 2 Fal 11:5,9]

Kudhulumiwa kwa watumwa

8Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, baada ya wakati ule mfalme Sedekia alipofanya agano na watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, kuwatangazia habari za uhuru;[#Kut 21:1; Law 25:10; Kum 15:12; Isa 1:17; Mik 2:1-3,7-13]

9ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake, na kila mtu amweke huru mjakazi wake, ikiwa yule mwanamume au yule mwanamke ni Mwebrania; mtu yeyote asiwatumikishe, yaani, asimtumikishe Myahudi, nduguye;[#Neh 5:11; Law 25:39]

10na wakuu wote, na watu wote, wakati, waliofanya agano hilo, ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake na mjakazi wake, mtu yeyote asiwatumikishe tena; wakatii, wakawaacha.

11Lakini baadaye wakaghairi, wakawarudisha watumwa wale, na wajakazi wale, ambao wamewaacha huru, nao wakawatia utumwani wawe watumwa na wajakazi wao.[#Yer 37:5; Hos 6:4]

12Basi, neno la BWANA likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,

13BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nilifanya agano na baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa, nikisema,

14Mwisho wa kila mwaka wa saba kila mtu na amwache huru ndugu yake aliye Mwebrania, aliyeuzwa kwako na kukutumikia miaka sita utamwacha atoke kwako huru, lakini baba zenu hawakunisikiliza, wala hawakutega masikio yao.[#Kut 21:2; Kum 15:12; Law 25:39]

15Na ninyi mlikuwa mmegeuka, mkafanya yaliyo haki machoni pangu, kwa kumtangazia uhuru kila mtu ndugu yake; nanyi mlikuwa mmefanya agano mbele zangu, katika nyumba ile iitwayo kwa jina langu;[#2 Fal 23:3; Neh 10:29; Yer 7:10]

16lakini mlighairi, na kulitukana jina langu; kila mtu akamrudisha mtumwa wake na mjakazi wake, ambao mmewaweka huru kama walivyopenda wenyewe, mkawatia utumwani tena, wawe watumwa wenu na wajakazi wenu.[#Kut 20:7; Law 19:12]

17Basi BWANA asema hivi, Hamkunisikiliza kumtangazia uhuru kila mtu ndugu yake, na kila mtu jirani yake; tazama, mimi nawatangazieni uhuru, asema BWANA, yaani, wa upanga, na njaa, na tauni; nami nitawatoa ninyi mtupwe huku na huko katika falme zote za dunia.[#Neh 9:30; Mt 7:2; Gal 6:7; 1 The 4:6; Yer 32:24,36]

18Na watu hao waliolivunja agano langu, wasioyatimiza maneno ya agano lile, walilolifanya mbele zangu, wakati ule walipomkata ndama vipande viwili, wakapita katikati ya vipande vile;[#Rum 2:8; Mwa 15:10; Zab 50:5]

19wakuu wa Yuda, na wakuu wa Yerusalemu, matowashi, na makuhani, na watu wote wa nchi, waliopita katikati ya vipande vile vya huyo ndama;

20mimi nitawatia katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta roho zao, na mizoga yao itakuwa ni chakula cha ndege wa mbinguni, na cha wanyama wakali wa nchi.[#Kum 28:26; Zab 79:2; Yer 7:33; 16:4; Ufu 19:17-21]

21Na Sedekia, mfalme wa Yuda, na wakuu wake nitawatia katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta roho zao, na katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, waliokwenda zao na kuwaacheni.[#Yer 37:5]

22Tazama, nitawapa amri yangu, asema BWANA, na kuwarejesha kwenye mji huu; nao watapigana nao, na kuutwaa, na kuuteketeza kwa moto; nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, isikaliwe na mtu.[#Amo 3:6; Yer 37:8; 38:3; 39:1,2,8; 9:11; 33:10; Mik 7:13; Zek 1:12]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya