Yeremia 48

Yeremia 48

Hukumu ya Moabu

1Kuhusu Moabu. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ole wake Nebo! Kwa maana umeharibika; Kiriathaimu umeaibishwa, umetwaliwa; Misgabu umeaibishwa, nao umebomolewa.[#Isa 15:1; Hes 32:38]

2Sifa za Moabu haziko tena; katika Heshboni wameazimia mabaya juu yake, Haya! Njooni, na tumkatilie mbali asiwe taifa. Wewe nawe, Ee Madmena, utanyamazishwa; upanga utakufuatia.

3Sauti ya kilio toka Horonaimu,

Ya kutekwa na uharibifu mkuu.

4Moabu umeharibika;

Wadogo wake wamelia kwa sauti.

5Kwa maana watu wapandapo huko Luhithi

Watapanda wasiache kulia;

Nao watu wateremkapo huko Horonaimu

Wameisikia huzuni ya kilio cha uharibifu.

6Haya! Kimbieni! Jiokoeni nafsi zenu!

Mkawe kama mtu aliye mkiwa.

7Maana, kwa kuwa umeyatumainia matendo yako, na hazina zako, wewe nawe utatwaliwa; na Kemoshi atatoka aende katika uhamisho, makuhani wake na wakuu wake pamoja.[#Zab 49:6,7; 52:7; Yer 9:23; 1 Tim 6:17; Ufu 18:17; Hes 21:29]

8Naye mwenye kuteka nyara atakuja juu ya kila mji, wala hakuna mji utakaookoka; bonde nalo litaangamia, nayo nchi tambarare itaharibiwa; kama BWANA alivyosema.

9Mpe Moabu mabawa, apate kuruka na kwenda zake; na miji yake itakuwa ukiwa, isiwe na mtu wa kukaa ndani yake.

10Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu.[#1 Sam 15:3]

11Moabu amestarehe tangu ujana wake, naye ametulia juu ya sira zake, wala hakumiminwa kutoka chombo kimoja kutiwa chombo kingine, wala hakwenda kufungwa; kwa hiyo ladha yake anakaa nayo, wala harufu yake haikubadilika.[#Sef 1:12]

12Basi, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo nitatuma kwake wamiminao, nao watammimina, nao watamwaga vyote vilivyomo vyomboni mwake, na kuzivunja chupa zake vipande vipande.

13Na Moabu ataona haya kwa ajili ya Kemoshi, kama nyumba ya Israeli ilivyoona haya kwa ajili ya Betheli, tegemeo lao.[#Amu 11:24; Hos 10:6; 1 Fal 12:29; Amo 5:5,6]

14Mwasemaje ninyi, Sisi tu mashujaa, watu hodari wa vita.[#Zab 33:6; Mhu 9:11; Isa 16:6; Yer 9:23]

15Moabu ameharibika, na moshi wa miji yake umepanda; na vijana wake wateule wameteremka kwenda kuchinjwa, asema Mfalme, ambaye jina lake ni BWANA wa majeshi.[#Yer 50:27; 51:57; Mal 1:14]

16Msiba wa Moabu umefika karibu,

Na mateso yake wanamjia haraka.

17Ninyi nyote mnaomzunguka, mlilieni,[#Isa 9:4; 14:4]

Nanyi nyote mlijuao jina lake, semeni,

Jinsi ilivyovunjika fimbo ya enzi,

Fimbo ile iliyokuwa nzuri!

18Ee binti ukaaye Diboni,[#Isa 47:1; 15:2; Yer 46:19; Hes 21:30]

Shuka toka utukufu wako, ukae katika kiu;

Maana atekaye Moabu amepanda juu yako,

Ameziharibu ngome zako.

19Wewe ukaaye Aroeri,[#Kum 2:36; 1 Sam 4:13,16]

Simama kando ya njia upeleleze;

Mwulize mwanamume akimbiaye na mwanamke atorokaye,

Sema, Imetendeka nini?

20Moabu ameaibishwa, kwa maana amevunjika;[#Hes 21:13]

Ombolezeni na kulia;

Tangazeni habari hii katika Arnoni,

Ya kuwa Moabu ameharibika.

21Na hukumu imeifikia nchi tambarare; juu ya Holoni, na juu ya Yasa, na juu ya Mefaathi;

22na juu ya Diboni, na juu ya Nebo, na juu ya Beth-diblathaimu;

23na juu ya Kiriathaimu, na juu ya Beth-gamuli, na juu ya Beth-meoni;

24na juu ya Keriothi, na juu ya Bozra, na juu ya miji yote ya nchi ya Moabu, iliyo mbali na iliyo karibu.[#Amo 2:2]

25Pembe ya Moabu imekatika, na mkono wake umevunjika, asema BWANA. Mlevyeni; kwa maana alijitukuza juu ya BWANA

26na Moabu atagaagaa katika matapiko yake, naye atadhihakiwa. Kwa maana Israeli, je! Hakuwa dhihaka kwako?[#Yer 25:15]

27Alionekana kati ya wezi? Maana kila umtajapo watikisa kichwa chako.[#Mit 24:17; Sef 2:8; Yer 2:26]

28Enyi mkaao Moabu, ondokeni mijini,[#Zab 55:6,7; Wim 2:14]

Nendeni mkakae majabalini;

Mkawe kama njiwa atengenezaye kiota chake

Kandoni mwa mdomo wa shimo.

29Tumesikia habari za kiburi cha Moabu;[#Isa 16:6]

Ya kuwa ana kiburi kingi;

Ujeuri wake, na kiburi chake, na majivuno yake,

Na jinsi alivyojitukuza moyoni mwake.

30Najua ghadhabu yake, asema BWANA, ya kuwa si kitu; majisifu yake hayakutenda neno lolote.

31Kwa sababu hiyo nitamwombolezea Moabu, naam, nitapiga kelele kwa ajili ya Moabu yote; nitawaombolezea watu wa Kir-heresi.[#Isa 15:5]

32Nitakulilia, Ee mzabibu wa Sibma, kwa vilio vipitavyo vilio vya Yazeri; matawi yako yalipita juu ya bahari, yalifika hadi bahari ya Yazeri; atekaye nyara ameyaangukia matunda yako ya wakati wa jua, na mavuno yako ya zabibu.[#Hes 21:13]

33Furaha na shangwe zimeondoshwa, katika shamba lizaalo sana, na katika nchi ya Moabu; nami nimeikomesha divai katika mashinikizo; hapana mtu atakayekanyaga zabibu kwa shangwe; shangwe ile itakuwa si shangwe.[#Isa 16:9,10; Yoe 1:12]

34Toka kilio cha Heshboni mpaka Eleale, naam, mpaka Yahasa, wametoa sauti zao, toka Soari mpaka Horonaimu, hata Eglath-shelishia; maana maji ya Nimrimu nayo yatakuwa ukiwa.[#Isa 15:4-6]

35Pamoja na hayo, asema BWANA, nitamkomesha katika Moabu mtu atoaye sadaka katika mahali pa juu, naye awafukiziaye uvumba miungu yake.[#Isa 15:2]

36Kwa sababu hiyo moyo wangu watoa sauti kama filimbi kwa ajili ya Moabu, na kwa ajili ya watu wa Kir-heresi, moyo wangu watoa sauti kama filimbi; kwa kuwa wingi aliojipatia umepotea.[#Mit 11:4; Mhu 5:13-14; Isa 15:7; Lk 12:20,21]

37Maana kila kichwa kina upara, na ndevu zote zimenyolewa; mikono yote ina alama za chale, na viuno vyote vimevikwa nguo za magunia.[#Yer 47:5; Mwa 37:34]

38Juu ya madari yote ya nyumba za Moabu, na katika njia kuu zake, pana maombolezo, kila mahali; kwa maana nimevunja Moabu kama chombo kisichopendeza, asema BWANA.[#Yer 22:28]

39Jinsi alivyovunjika! Ombolezeni! Jinsi Moabu alivyogeuza kisogo kwa haya! Hivyo ndivyo Moabu atakavyokuwa dhihaka, na sababu ya kuwashangaza watu wote wamzungukao.

40Maana BWANA asema hivi, Tazama, ataruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Moabu.[#Yer 49:22; Dan 7:4; Hos 8:1; Hab 1:8; Isa 8:8]

41Miji imetwaliwa, ngome zimeshambuliwa, na mioyo ya mashujaa wa Moabu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke akiwa katika uchungu wa kujifungua.[#Isa 13:8; Yer 30:6; Mik 4:9]

42Na Moabu ataangamizwa, asiwe taifa tena, kwa sababu alijitukuza juu ya BWANA.[#Zab 83:4; Isa 16:13,14; Mit 16:18]

43Hofu, na shimo, na mtego, zaja juu yako, Ee mwenyeji wa Moabu, asema BWANA.[#Isa 24:17,18]

44Aikimbiaye hofu ataanguka shimoni; na yeye atokaye shimoni atanaswa kwa mtego; maana nitaleta juu yake, yaani, juu ya Moabu, mwaka wa kujiliwa kwake, asema BWANA.[#Yer 11:23]

45Wamekimbia, wasio na nguvu[#Hes 21:28; 24:17]

Wanasimama chini ya kivuli cha Heshboni;

Ila moto umetoka katika Heshboni,

Na muali wa moto toka kati ya Sihoni

Nao umekula pembe ya Moabu,

Na utosi wa kichwa wa watu wapigao kelele.

46Ole wako! Ee Moabu,[#Hes 21:29; Amu 11:24]

Watu wa Kemoshi wamepotea;

Maana wana wako wamechukuliwa mateka,

Na binti zako wamekwenda utumwani.

47Lakini nitawarudisha watu wa Moabu walio utumwani, siku za mwisho, asema BWANA. Hukumu ya Moabu imefikia hapa.[#Yer 49:6,39]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya