Yeremia 50

Yeremia 50

Hukumu juu ya Babeli

1Neno hili ndilo alilosema BWANA, kuhusu Babeli na kuhusu Wakaldayo, kwa kinywa cha Yeremia, nabii.[#Isa 13:1; 21:1]

2Tangazeni katika mataifa,[#Isa 46:1; Yer 43:12]

Mkahubiri na kutweka bendera;

Hubirini, msifiche, semeni,

Babeli umetwaliwa!

Beli amefedheheka;

Merodaki amefadhaika;

Sanamu zake zimeaibishwa,

Vinyago vyake vimefadhaika.

3Maana toka kaskazini taifa linakuja juu yake, litakaloifanya nchi yake kuwa ukiwa; wala hakuna mtu atakayekaa humo; wamekimbia, wamekwenda zao, mwanadamu na mnyama pia.[#Isa 13:17]

4Katika siku hizo, na wakati huo, asema BWANA, wana wa Israeli watakuja, wao na wana wa Yuda pamoja; Wataendelea njiani mwao wakilia, nao watamtafuta BWANA, Mungu wao.[#Hos 1:11; 3:5; Zab 126:5; 105:4; Zek 12:10; 8:21,22; Isa 45:19]

5Watauliza njia ya kwenda Sayuni, na nyuso zao zitaelekea huko, wakisema, Njooni ninyi, mjiunge na BWANA, kwa agano la milele ambalo halitasahauliwa.[#Yer 31:31; 1 Pet 2:25]

6Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hadi kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika.

7Watu wote waliowaona wamewala; na adui zao walisema, Sisi hatuna hatia, kwa kuwa hao wametenda dhambi juu ya BWANA, aliye kao la haki, yaani, BWANA, tumaini la baba zao.[#Zek 11:5; Yer 2:3; Dan 9:16; Zab 22:4]

8Kimbieni kutoka kati ya Babeli, mkatoke katika nchi ya Wakaldayo, mkawe kama mabeberu mbele ya makundi.[#Ufu 18:4; Isa 48:20; Yer 51:6; Zek 2:6]

9Kwa maana juu ya Babeli nitaamsha na kuleta kusanyiko la mataifa makubwa, toka nchi ya kaskazini; nao watajipanga juu yake; kutoka huko atatwaliwa; mishale yao itakuwa kama ya mtu shujaa aliye stadi; hakuna hata mmoja utakaorudi bure.

10Nao Ukaldayo utakuwa mateka; wote wautekao watashiba, asema BWANA.[#Ufu 17:16]

11Kwa sababu mnafurahi, kwa sababu mnashangilia, enyi mnaouteka urithi wangu, kwa sababu mmenona kama mtamba akanyagaye nafaka, nanyi mnalia kama farasi wenye nguvu;[#Isa 47:6]

12mama yenu atatahayarika sana; yeye aliyewazaa atafadhaika; tazama, atakuwa taifa lililo nyuma katika mataifa yote, atakuwa jangwa, nchi ya ukame, na nyika.

13Kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote.

14Jipangeni juu ya Babeli pande zote,

Ninyi nyote mpindao upinde;

Mpigeni, msiuzuie hata mshale mmoja;

Kwa maana amemtenda BWANA dhambi.

15Mpigieni kelele pande zote; amejitoa;[#1 Nya 29:24; 2 Nya 30:8; Omb 5:6; Yer 51:58; Zab 137:8; Yak 2:13; Ufu 16:6]

Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa;

Kwa maana ni kisasi cha BWANA; mlipizeni kisasi;

Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye.

16Mpanzi mkatilie mbali na Babeli,[#Isa 13:14]

Naye ashikaye mundu wakati wa mavuno;

Kwa sababu ya kuuogopa upanga uoneao,

Watageuka kila mtu kwa watu wake,

Nao wataikimbilia kila mmoja nchi yake.

17Israeli ni kondoo aliyetawanywa; simba wamemfukuzia mbali; kwanza mfalme wa Ashuru amemla, na mwisho Nebukadneza huyu, mfalme wa Babeli, amemvunja mifupa yake.[#Yoe 3:12; Mt 9:36; Yer 23:2; 2:15; 1 Pet 2:25; 2 Nya 28:20; 2 Fal 17:6; 24:10,14; Isa 7:17,20; 8:7,8]

18Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, mimi nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.

19Nami nitamleta Israeli tena malishoni kwake, naye atalisha juu ya Karmeli, na Bashani, na nafsi yake itashiba juu ya milima ya Efraimu, na katika Gileadi.[#Isa 65:10]

20Katika siku hizo na wakati huo, asema BWANA, uovu wa Israeli utatafutwa, wala hakuna uovu; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana; maana nitawasamehe wale niwaachao kuwa mabaki.[#Yer 31:34; Isa 1:9]

21Panda juu ya nchi ya Merathaimu, naam, juu yake, na juu yao wakaao Pekodi; ua, ukaangamize nyuma yao, asema BWANA, ukatende kama nilivyokuagiza, yote pia.[#Isa 10:6]

22Kuna kishindo cha vita katika nchi,

Kishindo cha uharibifu mkuu.

23Imekuwaje nyundo ya dunia yote[#Isa 16:6; Yer 51:20]

Kukatiliwa mbali na kuvunjwa?

Imekuwaje Babeli kuwa ukiwa

Katikati ya mataifa?

24Nimekutegea mtego, Ee Babeli, nawe ukanaswa, nawe ulikuwa huna habari; umeonekana, ukakamatwa, kwa sababu ulishindana na BWANA.[#Dan 5:30]

25BWANA amefungua akiba yake ya silaha, naye amezitoa silaha za ghadhabu yake; maana Bwana, BWANA wa majeshi, ana kazi atakayofanya katika nchi ya Wakaldayo.[#Isa 13:5]

26Njooni juu yake toka mpaka ulio mbali;

Zifungueni ghala zake;

Mfanyeni kuwa magofu na kumharibu kabisa;

Msimsazie kitu chochote.

27Wachinjeni mafahali wake wote;[#Zab 22:12; Isa 34:7; Yer 48:44]

Na wateremkie machinjoni;

Ole wao! Maana siku yao imewadia,

Wakati wa kujiliwa kwao.

28Sauti yao wakimbiao na kuokoka,[#Yer 51:10]

Kutoka katika nchi ya Babeli,

Ili kutangaza katika Sayuni kisasi cha BWANA, Mungu wetu,

Kisasi cha hekalu lake.

29Waiteni wapiga mishale juu ya Babeli,[#Ufu 18:6; Omb 3:64; 2 The 1:6; Isa 47:10]

Naam, wote waupindao upinde;

Pangeni hema kumzunguka pande zote;

Ili asiokoke hata mtu mmoja wao;

Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake;

Mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda;

Kwa sababu amefanya kiburi juu ya BWANA,

Juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.

30Kwa sababu hiyo vijana wake wataanguka katika njia zake kuu, na watu wake wa vita, wote pia, watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA.[#Yer 49:26; 51:4]

31Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, BWANA wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujia.

32Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote.[#Yer 21:14]

33BWANA wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda wameonewa sana, na pia wana wa Yuda vivyo hivyo, watekaji wao wote wamewashikilia sana; na wamekataa kuwaachilia waondoke.

34Mkombozi wao ni hodari; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli.[#Ufu 18:8; Mit 23:11; Isa 47:4]

35Upanga uko juu ya Wakaldayo, asema BWANA, na juu yao wakaao Babeli, na juu ya wakuu wake, na juu ya watu wake wenye hekima.[#Dan 5:30; Isa 37:13]

36Upanga uko juu ya hao wajisifuo, nao watapumbazika; upanga uko juu ya mashujaa wake, nao watafadhaika.

37Upanga uko juu ya farasi wao, na juu ya magari yao ya vita; na juu ya watu wote waliochanganyika ndani yake, nao watakuwa kama wanawake; upanga u juu ya hazina zake, nazo zitaibwa.[#Yer 25:20; 51:30; Nah 3:13]

38Ukosefu wa mvua uko juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu.[#Isa 44:27; Ufu 16:12; Yer 51:32,36]

39Basi, wanyama wakali wa jangwani, pamoja na mbwamwitu, watakaa huko, na mbuni watakaa ndani yake; wala haitakaliwa na watu milele; wala hakuna mtu atakayekaa huko tangu kizazi hadi kizazi.[#Ufu 18:2; Isa 13:21; Yer 51:37; 25:12]

40Kama vile ilivyotokea Mungu alipoangusha Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; kadhalika hakuna mtu atakayekaa huko, wala hakuna mwanadamu atakayekaa huko kama wageni wakaavyo.[#Mwa 19:24-25; Kum 29:23; Isa 1:9; Yer 49:18; Amo 4:11; Sef 2:9; 2 Pet 2:6; Yud 1:7]

41Angalia, watu wanakuja watokao kaskazini; na taifa kubwa, na wafalme wengi wataamshwa toka pande za mwisho za dunia.[#Yer 6:22; Ufu 17:16]

42Wanashika upinde na mkuki;[#Isa 13:18; 5:30]

Ni wakatili, hawana huruma;

Sauti yao inanguruma kama bahari,

Nao wamepanda farasi;

Kila mmoja amejipanga kama aendaye vitani,

Juu yako, Ee binti Babeli.

43Mfalme wa Babeli amesikia habari zao,[#Yer 49:24]

Na mikono yake imekuwa dhaifu;

Dhiki imemshika, na maumivu,

Kama ya mwanamke akiwa katika uchungu wa kujifungua.

44Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafla ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?[#Ayu 41:10; Dan 5:2,20]

45Basi, lisikieni shauri la BWANA,[#Zab 33:11; Isa 14:24; Yer 51:11; Mdo 4:28; Efe 1:11; 1 Kor 1:27]

Alilolifanya juu ya Babeli;

Na makusudi yake aliyoyakusudia

Juu ya nchi ya Wakaldayo.

Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi;

Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.

46Kwa kishindo cha kutwaliwa Babeli nchi itatetemeka,[#Ufu 18:9]

Na kilio chake chasikiwa katika mataifa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya