Yohana 20

Yohana 20

Kufufuka kwa Yesu

1Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kukiwa bado giza; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini.[#Mt 28:1-10; Mk 16:1-11; Lk 24:1-12]

2Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka.[#Yn 13:23]

3Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini.

4Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza kufika kaburini.

5Akainama na kuchungulia, akaona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia.

6Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala,

7na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwazongwa mbali mahali peke yake.[#Yn 11:44]

8Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza kufika kaburini, akaona na kuamini.

9Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka.[#1 Kor 15:4; Mdo 2:24-32]

10Basi wale wanafunzi wakaenda zao tena nyumbani kwao.

Yesu amtokea Mariamu Magdalene

11Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Wakati alipokuwa akilia, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi.

12Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu.

13Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka.

14Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu.

15Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.

16Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu wangu).

17Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.[#Ebr 2:11,12; Rum 8:29]

18Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.

Yesu awatokea wanafunzi

19Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu.[#Mk 16:14-18; Lk 24:36-49]

20Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.[#1 Yoh 1:1]

21Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.[#Yn 17:18]

22Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.[#Mwa 2:7]

23Na wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.[#Mt 16:19; 18:18]

Yesu na Tomaso

24Lakini mmoja wa wale Kumi na Wawili, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu.[#Yn 11:16; 14:5]

25Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.[#Yn 19:34]

26Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu.[#Yn 20:19]

27Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.

28Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu![#Yn 1:1]

29Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.[#1 Pet 1:8]

Lengo la kitabu hiki

30Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki.

31Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini muwe na uzima kwa jina lake.[#1 Yoh 5:13; Rum 1:17]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya