The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Elifazi, Mtemani, akajibu, na kusema,
2Je! Yapasa mtu mwenye hekima kujibu kwa ujuzi wa uvuvio,
Na kulijaza tumbo lake upepo wa mashariki?
3Je! Ahoji na mazungumzo yasiyo na faida,
Au kwa maneno ambayo hawezi kufanya mema kwayo?
4Naam, wewe wapuuza hofu ya Mungu,
Nawe wazuia ibada mbele za Mungu.
5Kwani uovu wako unakufundisha kinywa chako,
Nawe wachagua ulimi wake mwenye hila.
6Kinywa chako mwenyewe chakuhukumia makosa, wala si mimi;
Naam, midomo yako mwenyewe hushuhudia juu yako.
7Je! Wewe u mtu wa kwanza aliyezaliwa?[#Mit 8:25]
Au, ulizawa wewe kabla ya milima?
8Je! Umesikiza ushauri wa siri ya Mungu?[#Mt 11:25; Rum 11:34; 1 Kor 2:11]
Nawe je! Wazuia hekima iwe yako tu?
9Je! Wewe wajua neno lipi, ambalo sisi hatulijui?[#Ayu 13:2]
Nawe wafahamu nini, ambalo halimo ndani yetu?
10Wenye mvi, na walio wazee sana, wote wapo pamoja nasi,[#Kum 32:7; Ayu 8:8-10; Mit 16:31]
Ambao ni wazee kuliko baba yako.
11Je! Utulivu wa Mungu ni mdogo sana kwako,
Maliwazo ya Mungu ni madogo sana kwako?
12Mbona moyo wako unakutaharakisha!
Na macho yako, je! Kwa nini yaangae?
13Hata ukageuza roho yako kinyume cha Mungu,
Na kuyatoa maneno kama hayo kinywani mwako.
14Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi?[#Ayu 25:4-6; 14:4; Zab 14:3; Mit 20:9; Mhu 7:20; Rum 7:18; Efe 2:2,3]
Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki?
15Yeye hawategemei watakatifu wake;[#Ayu 25:5]
Naam, mbingu nazo si safi machoni pake.
16Sembuse mtu ambaye ni mwenye kuchukiza na uchafu,[#Zab 14:3; Mit 19:28]
Mwanadamu anywaye uovu kama anywavyo maji!
17Mimi nitakuonesha, unisikilize;
Na hayo yote niliyoyaona nitayanena;
18(Ambayo watu wenye hekima wameyatangaza[#Mwa 18:19]
Tokea baba zao, wala hawakuyaficha;
19Waliopewa hiyo nchi peke yao,[#Yoe 3:17]
Wala mgeni hakupita kati yao);
20Mtu mwovu huwa na uchungu siku zake zote,[#Zab 90:12]
Hata hesabu ya miaka aliyowekewa mwonevu.
21Sauti za utisho zi masikioni mwake;[#1 The 5:3]
Katika kufanikiwa kwake mtekaji nyara atamjia juu yake;
22Yeye hasadiki kwamba atarudi kutoka gizani,
Naye hungojewa na upanga;
23Hutangatanga ili apate chakula, akisema, Ki wapi?[#Zab 59:15; Ayu 18:12]
Ajua kwamba siku ya giza i tayari karibu naye;
24Mateso na dhiki humtia hofu;
Humshinda kama vile mfalme aliye tayari kwa vita;
25Kwa kuwa amenyosha mkono wake juu ya Mungu,[#Mal 3:13]
Na kuendelea kwa kiburi kinyume cha Mwenyezi;
26Humshambulia na shingo ngumu,
Kwa mafundo makubwa ya ngao zake;
27Kwa kuwa amefunika uso wake na mafuta yake,[#Zab 17:10]
Na kuwandisha mafuta kiunoni mwake;
28Naye amekaa katika miji iliyo ukiwa,
Katika nyumba ambazo hapana mtu azikaaye,
Zilizokuwa tayari kuwa magofu.
29Hatakuwa tajiri, wala mali zake hazitadumu,
Wala mavuno yao hayatainama nchi.
30Hataondoka gizani;[#Ayu 4:9; Isa 11:4; Ufu 19:15]
Ndimi za moto zitayakausha matawi yake,
Naye ataondoka kwa pumzi za kinywa chake.
31Asiutumainie ubatili, na kujidanganya;[#Zab 62:10; Isa 59:4]
Kwa kuwa huo ubatili ndio utakaokuwa ujira wake.
32Jambo hili litatendeka kabla ya wakati wake,[#Ayu 22:16; Zab 55:23]
Na tawi lake halitasitawi.
33Atayapukutisha mapooza yake kama mzabibu,
Na kuyatupa maua yake kama mzeituni.
34Kwa kuwa jamii ya hao wasiomcha Mungu watakuwa tasa,[#Isa 33:14]
Na moto utateketeza mahema yenye rushwa.
35Wao hutunga mimba ya madhara, na kuzaa uovu,[#Zab 7:14; Isa 59:4]
Na mioyo yao hutunga udanganyifu.