Ayubu 18

Ayubu 18

Bildadianena: Mungu huwaadhibu waovu

1Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema,

2Je! Hata lini utayawinda maneno kwa mitego?

Fikiri, kisha baadaye tutanena.

3Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani,[#Ayu 12:7; Zab 73:22]

Tena kuwa wanajisi machoni pako?

4Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako,[#Ayu 13:14]

Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe?

Au jabali litaondolewa mahali pake?

5Naam, mwanga wa waovu utazimika,[#Ayu 21:17; Mit 13:9]

Wala muali wa moto wake hautang'aa.

6Mwanga hemani mwake utakuwa giza,

Nayo taa iliyo juu yake itazimwa.

7Hatua zake za nguvu zitasongwa,

Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini.

8Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe,

Naye huenda juu ya matanzi.

9Tanzi litamshika kisigino chake,

Na mtego utamshika.

10Amefichiwa tanzi chini,

Na mtego amewekewa njiani.

11Vitisho vitamtia hofu kutoka kila upande,[#Ayu 6:4; Zab 73:19; Yer 6:25; 2 Kor 5:11]

Na kumfukuza karibu na visigino vyake.

12Nguvu zake zitaliwa na njaa,[#Ayu 15:23; 1 The 5:3]

Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake.

13Utakula via vya mwili wake,

Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake.

14Atang'olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini;[#Ayu 8:14; Zab 112:10; Mit 10:28; Mt 7:26,27]

Naye atapelekwa kwake mfalme wa vitisho.

15Katika hema yake hakuna kitakachobaki;[#Mwa 19:24]

Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake.

16Chini, mizizi yake itakaushwa;

Na juu, tawi lake litasinyaa.

17Kumbukumbu lake litakoma katika nchi,[#Zab 34:16; Mit 2:22]

Wala hatakuwa na jina mashambani.

18Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani,

Na kufukuzwa atoke duniani.

19Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake,[#Isa 14:22; Yer 22:30]

Wala hatasalia mtu hapo alipokaa.

20Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake,

Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu.

21Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu,[#Yer 9:3; 1 The 4:5; 2 The 1:8; Tit 1:16]

Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya