The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Sofari, Mnaamathi, akajibu, na kusema,
2Kwa hiyo mawazo yangu hunipa jawabu,
Kwa ajili ya haraka niliyo nayo ndani yangu.
3Nimesikia maonyo yanayonitahayarisha,
Nayo roho ya ufahamu wangu hunijibu.
4Je! Hujui neno hili tangu zamani za kale,
Tangu wanadamu kuwekwa juu ya nchi,
5Ya kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo,[#Zab 37:35]
Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu?
6Ujapopanda ukuu wake mpaka mbinguni,
Na kichwa chake kufikia mawinguni;
7Hata hivyo ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe;
Hao waliomwona watasema, Yuko wapi?
8Ataruka mfano wa ndoto, asionekane;
Naam, atafukuzwa kama maono ya usiku,
9Jicho lililomwona halitamwona tena;
Wala mahali pake hapatamtazama tena.
10Watoto wake watataka fadhili kwa maskini,
Na mikono yake itarudisha mali yake.
11Mifupa yake imejaa ujana wake,
Lakini utalala nchi naye mavumbini.
12Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake,
Ingawa auficha chini ya ulimi wake;
13Ingawa hawataki kuuachilia uende zake.
Naye huushikilia kinywani mwake;
14Hata hivyo chakula chake matumboni mwake kinabadilika,[#Yer 4:18]
Kimekuwa ni nyongo za majoka ndani yake.
15Amemeza mali, naye atayatapika tena;[#Mt 27:3,4]
Mungu atayatoa tumboni mwake.
16Atanyonya sumu ya majoka;
Na ulimi wa fira utamwua.
17Hataiangalia hiyo mito ya maji,[#Yer 17:6]
Vile vijito vilivyojaa asali na siagi.
18Aliyoyataabikia kazi atayarudisha, asiyameze;
Kwa mali aliyoyapata, hatafurahi.
19Kwa maana amewaonea na kuwaacha maskini;
Amenyang'anya nyumba kwa jeuri, wala hataijenga.
20Kwa sababu hakujua utulivu ndani yake,[#Mhu 5:13]
Hataokoa chochote kutoka hicho alichokifurahia.
21Hakikusalia kitu asichokula;
Kwa hiyo kufanikiwa kwake hakutadumu.
22Katika kujaa kwa wingi wake atakuwa katika dhiki;
Mkono wa kila anayesumbuliwa utamjia.
23Hapo atakapo kulijaza tumbo lake,[#Hes 11:33; Zab 78:30,31]
Mungu atamtupia ukali wa ghadhabu zake,
Na kuunyesha juu yake akiwa anakula.
24Ataikimbia silaha ya chuma,[#Isa 24:18; Yer 48:43; Amo 5:19]
Na uta wa shaba utamchoma.
25Yeye autoa, nao watoka mwilini mwake;[#Ayu 18:11; Zab 73:19]
Naam, ncha ing'aayo yatoka katika nyongo yake;
Vitisho viko juu yake.
26Giza lote linawekwa kwa ajili ya hazina zake;[#Zab 21:9]
Moto ambao haukuvuviwa na mtu utamla;
Utayateketeza yaliyosalia hemani mwake.
27Mbingu zitafunua wazi uovu wake,[#Isa 26:21]
Nayo nchi itainuka kinyume chake.
28Mali ya nyumba yake yatanyakuliwa,
Yatamwagika mbali katika siku ya ghadhabu zake.
29Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu itokayo kwa Mungu,[#Kum 29:20,28; Ayu 18:21; 27:13; Zab 11:5,6; Mt 24:51]
Na urithi aliowekewa na Mungu.