Ayubu 40

Ayubu 40

1BWANA akafululiza kumjibu Ayubu, na kusema,

2Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi?[#Ayu 9:3; Isa 45:9]

Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye.

Jibu la Ayubu kwa Mungu

3Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema,

4Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini?[#Ezr 9:6; Zab 51:4; Ayu 29:9; Zab 39:9; Zek 2:13]

Naweka mkono wangu kinywani pangu.

5Nimenena mara moja, nami sitajibu;

Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.

Mungu amchochea Ayubu

6Ndipo BWANA akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema,[#Ayu 38:1; Zab 50:3]

7Jifunge viuno kama mwanamume,[#Ayu 38:3; 42:4]

Mimi nitakuuliza neno, nawe niambie.

8Je! Hata hukumu yangu utaibatilisha?[#Zab 51:4]

Utanitia mimi hatiani, upate kuhesabiwa haki?

9Au je! Wewe una mkono kama Mungu?[#Ayu 37:4; Zab 29:3]

Waweza kutoa ngurumo kwa sauti kama yeye?

10Haya! Jivike sasa fahari na ukuu;[#Zab 93:1]

Jipambe heshima na enzi.

11Mwaga mafuriko ya hasira zako,

Ukamtazame kila mtu mwenye kiburi, ukamdhalilishe.

12Mtazame kila mtu mwenye kiburi ukamshushe,[#Isa 2:12; Dan 4:37; Lk 18:14]

Ukawakanyage waovu hapo wasimamapo.

13Wafiche mavumbini pamoja,

Wafunge nyuso zao mahali palipositirika.

14Ndipo mimi nami nitazikiri habari zako,

Ya kuwa mkono wako wa kulia waweza kukuokoa.

15Mwangalie huyo kiboko, niliyemwumba pamoja nawe;

Yeye hula nyasi kama ng'ombe,

16Tazama basi, nguvu zake zimo katika viuno vyake,

Na uwezo wake u katika mishipa ya tumbo lake.

17Yeye hutikisa mkia wake mfano wa mwerezi;

Mishipa ya mapaja yake yanaungamana pamoja.

18Mifupa yake ni kama mirija ya shaba;

Mbavu zake ni kama vipande vya chuma.

19Yeye ni wa kwanza kwa hayo matendo makuu ya Mungu;

Ni Muumba wake tu awezaye kumkabili kwa upanga wake.

20Hakika milima humtolea chakula;[#Zab 104:14]

Hapo wachezapo wanyama pori wote.

21Hulala chini ya miti yenye vivuli,

Mafichoni penye mianzi, na matopeni.

22Hiyo miti yenye vivuli humfunika kwa vivuli vyao;

Mierebi ya vijito humzunguka.

23Tazama, mto ukifurika, yeye hatetemeki;[#Mwa 13:10; Yer 12:5]

Hujiona yu salama, ijapokuwa Yordani hufurika hata kinywani pake.

24Je! Mtu yeyote atamnasa akiwa yu macho,

Au, kumtoboa pua yake kwa mtego?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya