The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Ayubu akamjibu BWANA, na kusema.
2Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote,[#Yer 32:17; Mt 3:9; Mk 14:36; Lk 1:37; Efe 3:20]
Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.
3Ni nani huyu afichaye ushauri bila maarifa?[#Ayu 38:2; 1 Tim 1:7; Zab 40:5]
Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu,
Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua.
4Sikiliza, nakusihi, nami nitanena;[#Ayu 38:3]
Nitakuuliza neno, nawe niambie.
5Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio;[#Rum 10:17; Hes 12:8,9; Isa 6:1]
Bali sasa jicho langu linakuona.
6Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu
Katika mavumbi na majivu.
7Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
8Basi sasa, jitwalieni ng'ombe dume saba, na kondoo dume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende kulingana na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.[#Hes 23:1; Ebr 10:4; Mt 5:24; Mwa 20:17; Ebr 7:25; Yak 5:16]
9Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda, wakafanya kama vile BWANA alivyowaamuru; naye BWANA akamridhia Ayubu.
10Kisha BWANA akamrejeshea Ayubu mali yake, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.[#Ayu 1:1-3; Isa 40:2]
11Ndipo wakamwendea ndugu zake wote, wanaume kwa wanawake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakampa pole na kumliwaza kwa ajili ya mateso hayo yote aliyoleta BWANA juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja.[#Ayu 19:13]
12Basi hivyo BWANA akaubariki huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu moja, na punda wake elfu moja.[#Ayu 8:7; 1:3]
13Tena alikuwa na watoto wa kiume saba, na binti watatu.
14Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu.
15Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao wa kiume.
16Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia moja na arubaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hadi kizazi cha nne.[#Ayu 5:26]
17Basi Ayubu akafa, akiwa mzee sana mwenye kujawa na siku.[#Mwa 25:8]