Mambo ya Walawi 13

Mambo ya Walawi 13

Aina za ukoma na dalili zake

1Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2Mtu atakapokuwa na uvimbe katika ngozi ya mwili wake, au upele, au kipaku king'aacho, nao ukawa ni ugonjwa wa ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa mmojawapo wa wanawe makuhani;[#Kum 28:27; Isa 3:17; Law 10:10,11; Kum 17:8,9; Eze 22:26; Mal 2:7; Mt 8:2-4; 10:8; Lk 17:11-16; Yn 13:8-10]

3na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na nywele zilizoko katika hilo pigo zimegeuka kuwa nyeupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na ikiwa nywele zilizoko katika sehemu zilizougua zimegeuka rangi na kuwa nyeupe, na hilo pigo kuonekana limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili, hilo ni pigo la ukoma,[#13:3 Au ugonjwa.]

4Lakini ikiwa kipaku king'aacho katika ngozi ya mwili wake ni cheupe, na kuonekana si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi wala nywele hazikugeuka kuwa nyeupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo;

5kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limezuilika, na halikuenea katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena;

6kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikuwa katika ngozi yake ndipo kuhani atasema kuwa ni mzima, ni kipele tu; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa ni safi.[#Law 11:25; 14:8]

7Lakini ikiwa kipele kimeenea katika ngozi yake baada ya kujionesha kwa kuhani ili kutakaswa, atamwendea kuhani tena;

8naye kuhani ataangalia, ikiwa huo upele umeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa ni najisi; ni ukoma.[#2 Sam 3:29]

9Mtu atakapopatwa na ugonjwa wa ukoma, ndipo ataletwa kwa kuhani;[#2 Fal 5:3]

10naye kuhani ataangalia, ikiwa pana uvimbe mweupe katika ngozi yake, na mnywele zimegeuzwa kuwa nyeupe, tena ikiwa panafanyika kidonda katika ule uvimbe,[#Mk 1:44; Lk 5:14; 17:14; Hes 12:10,12; 2 Fal 5:27; 2 Nya 26:19,20]

11ni ukoma usiopona ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa ni najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye ana unajisi.

12Huo ukoma ukitokeza katika ngozi ya mgonjwa, na ukaenea katika ngozi yake yote, kutoka kichwani hadi miguuni, kama kuhani atakavyoweza kuona,

13ndipo huyo kuhani ataangalia; ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa ni safi huyo aliye na hilo pigo, ikiwa ngozi yake yote imegeuka kuwa nyeupe, naye akawa safi.

14Lakini popote kitakapoonekana kidonda kibichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi.

15Kuhani atakiangalia hicho kidonda kibichi, naye atasema kuwa ni najisi; kile kidonda kibichi ni najisi; ni ukoma.[#Kum 24:8]

16Au kama hicho kidonda kibichi kinageuka tena na kuwa cheupe, ndipo atamwendea kuhani,[#Lk 5:12-14; #13:16 weupe ni ishara ya kupona kwa kidonda.]

17na huyo kuhani atamwangalia; ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa huyo aliyekuwa na pigo ni safi.[#Kum 32:39; Zab 147:3]

18Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa,[#Kut 9:9; 15:26; Zab 38:3-7; Isa 38:21; Kum 28:27; 2 Fal 20:7; Ayu 2:7]

19na mahali palipokuwa na lile jipu pana uvimbe mweupe, au kipaku king'aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonesha kuhani mahali hapo;

20na kuhani ataangalia, kama kutaonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu.

21Lakini kuhani akipaangalia, na iwe hamna nywele nyeupe ndani yake, wala hapakuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

22na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi; hili ni pigo.

23Lakini ikiwa kipaku hicho king'aacho kimekaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi.[#Mit 28:13; Mt 8:4; Lk 5:14; 17:14; 1 Kor 5:5; Gal 6:1; 1 Pet 4:2,3]

24Au mwili wa mtu ukiwa una mahali palipoungua katika ngozi yake, kisha pakawa kidonda, kikawa kipaku chekundu kidogo, au cheupe;

25ndipo kuhani atapaangalia; ikiwa nywele iliyo katika kile kipaku imegeuka kuwa nyeupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali palipoungua; na kuhani atasema kuwa ni najisi; hili ni pigo la ukoma.[#Kut 4:6,7; Hes 12:10; 2 Sam 3:29; 2 Fal 5:27; 2 Nya 26:19; Mt 8:1-3; Mk 1:40-42; Lk 5:12-14]

26Lakini kuhani akipaangalia, nywele nyeupe hamna katika hicho kipaku king'aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

27na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kuwa ni najisi; hili ni pigo la ukoma.[#Law 10:10; Yer 15:19; Eze 22:26]

28Na kama hicho kipaku kikibaki pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kuwa ni safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili.

29Mwanamume au mwanamke atakapopatwa na maradhi kichani au kidevuni,

30ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; ikiwa pigo limeingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na nywele zilizomo kuwa za rangi ya manjano na nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi, maana ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa au wa kindevu.[#Kum 24:8; Mal 2:7; 1 Kor 12:9; Kum 28:27; Isa 3:17]

31Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, ikiwa kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba;

32na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe,

33ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena;[#Ayu 1:20; Rum 8:13]

34na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba ni safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa ni safi.

35Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake;

36ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye ni najisi.

37Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimepungua, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi.[#Law 10:10; Yer 15:19; Eze 22:26; 44:23]

38Mwanamume au mwanamke, atakapokuwa na vipaku ving'aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving'aavyo vyeupe;

39ndipo kuhani ataangalia; ikiwa vile vipaku ving'aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba iliyotokeza katika ngozi; yeye ni safi.

40Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upara, ni safi.[#Isa 15:2; Amo 8:10]

41Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upara wa kipaji; ni safi.

42Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upara, au kile kipaji kilicho na upara, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upara, au katika kipaji chake cha upara.

43Ndipo kuhani atamwangalia; kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu chekundu, katika kichwa chake chenye upara, au katika kipaji chake cha upara, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili;[#Law 10:10; Eze 22:26]

44yeye ni mtu mwenye ukoma, ni najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa ni najisi; pigo lake liko katika kichwa chake.

45Mtu mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, atavaa nguo zilizoraruka, na nywele timutimu; na ataufunika mdomo wake wa juu na kusema, “Ni najisi, ni najisi”.[#Eze 24:17,22; Mik 3:7; 1 Fal 8:37; Ayu 40:4; 42:6; Isa 6:5; Zab 61:1; 72:12; Lk 17:12,13; Ufu 21:4]

46Kwa siku zote ambazo pigo litakuwa ndani yake atakuwa najisi, ataishi kwa upweke katika makazi yake, nje ya kambi.[#Hes 5:2; 12:14; 2 Fal 7:3; 15:5; 2 Nya 26:21; Lk 17:12; 1 Kor 5:5; 2 The 3:6; Ebr 12:15]

47Kuhusu mavazi; vazi ambalo pigo la ukoma limo ndani yake, liwe ni vazi la sufu au la katani;[#Isa 59:6; 64:6; Eze 16:16; Zek 3:4; Rum 1:21-31; Yud 1:23]

48likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; liwe katika ngozi, au kitu chochote kilichofanywa cha ngozi;

49hilo pigo likiwa la rangi ya kijani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataoneshwa kuhani;

50na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba;[#Yer 15:19; Eze 44:23]

51kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yoyote; hilo pigo ni ukoma unaona; vazi hilo ni najisi.[#Law 14:44; Eze 16:43]

52Naye ataliteketeza vazi hilo, liwe ni la kufumwa au ni la kusokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu chochote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaona; vazi hilo litateketezwa;

53Na kama kuhani akitazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu chochote cha ngozi;

54ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena;

55kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, ni najisi; utaliteketeza; ni uharibifu likiwa lina doa ndani au nje.

56Huyo kuhani ataangalia, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa;

57kisha, likionekana liko vile vile katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utaliteketeza.

58Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu chochote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi.

59Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya