The chat will start when you send the first message.
1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za BWANA, ambazo mtazitangaza kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu.[#Kut 32:5; Hes 10:2,3,10; 2 Nya 30:5; Yoe 1:14; 2 Fal 10:20; Zab 81:3]
3Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yoyote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote.[#Kut 20:8-10; 23:12; 31:15; 34:21; 35:2; Kum 5:12-14; Lk 13:14; Neh 13:22; Isa 56:2; 58:13; Eze 20:12]
4Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayatangaza kwa nyakati zake.[#Kut 23:14]
5Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni Pasaka ya BWANA.[#Kut 12:1-13; Kum 16:1-2; Hes 28:16; Yos 5:10]
6Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.[#Kut 12:14-20; 23:15; 34:18; Kum 16:3-8]
7Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yoyote ya utumishi.[#Kut 12:16; Hes 28:18; Kum 16:1]
8Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi.
9Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
10Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;[#Kut 23:16; Hes 15:2,18; Kum 16:9; Yos 3:15; Mit 3:9; Rum 11:16; 1 Kor 15:20; Yak 1:18; Ufu 14:4]
11naye atautikisa mganda mbele za BWANA ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.[#Kut 29:24; Law 9:21; 10:14]
12Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume asiye na dosari wa mwaka wa kwanza, awe sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA.
13Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.
14Nanyi msile mkate, bisi, au masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hadi mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote.
15Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba;[#Kut 23:16; 34:22; Kum 16:9-12; Law 25:8]
16hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsogezea BWANA sadaka ya unga mpya.[#Mdo 2:1]
17Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa BWANA.[#Kut 23:16; 22:29; Hes 15:17-19; Kum 26:1,2]
18Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, wasio na dosari, wa mwaka wa kwanza, na ng'ombe dume mmoja, na kondoo wawili wa kiume; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
19Nanyi mtasongeza mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili wa kiume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani.[#Law 4:23,28; Hes 28:30]
20Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa BWANA, wawe wa huyo kuhani.[#Hes 18:12; Law 7:31-34; Kum 18:4]
21Nanyi mtatangaza suku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yoyote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu.
22Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Law 19:9-10; Kum 24:19-22; Kut 23:11; Kum 15:1-18; Ayu 20:19; Zab 112:9; Mit 14:31; Isa 58:7,8; Yak 2:1; Rut 2:15,16]
23Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
24Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu.[#Hes 10:10; 29:1; Law 25:9]
25Msifanye kazi yoyote ya utumishi; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto.
26Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,[#Law 16:29-34]
27Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtajinyima; na mtatoa sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto.[#Kut 30:10; Law 16:30; Hes 29:7; Isa 58:3,5; Dan 10:3,12]
28Na msifanye kazi yoyote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za BWANA, Mungu wenu.
29Kwa kuwa mtu yeyote asiyejinyima siku iyo hiyo, atatengwa na watu wake.[#Mwa 17:14; Law 13:46; Hes 5:2; 2 Nya 26:21; 2 The 3:6]
30Na mtu yeyote afanyaye kazi ya namna yoyote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake.
31Msifanye kazi ya namna yoyote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote.
32Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtajinyima; siku ya tisa ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hadi jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.
33Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,[#Kum 16:13-15]
34Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa BWANA.[#Kut 23:16; 34:22; Hes 29:12; Kum 16:13; Ezr 3:4; Neh 8:14; Zek 14:16; Yn 7:2; Ebr 11:9]
35Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi.
36Mtamsogezea BWANA sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamtolea BWANA sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yoyote ya utumishi.[#Hes 29:35; 2 Nya 7:8,9; Neh 8:18; Yn 7:37]
37Sikukuu za BWANA ni hizi, ambazo mtazipiga mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee BWANA sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake;
38zaidi ya hizo Sabato za BWANA, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa BWANA.
39Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, mtakapoyachuma mavuno ya nchi, mtasherehekea sikukuu ya BWANA kwa muda wa siku saba; siku ya kwanza na ya nane zitakuwa za kustarehe kabisa.[#Kut 23:16; Kum 16:13; Mt 21:8]
40Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, muda wa siku saba.[#Neh 8:15; Kum 16:14; Isa 35:10; 66:10; Rum 5:11]
41Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa BWANA muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba.
42Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazaliwa wote wa Israeli watakaa katika vibanda;
43ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwafanya wana wa Israeli kukaa katika vibanda, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri; mimi ndimi BWANA Mungu wenu.[#Kum 31:13; Zab 78:5,6]
44Naye Musa akawaambia wana wa Israeli hizo sikukuu za BWANA.