The chat will start when you send the first message.
1Na watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha Torati ya Musa, BWANA aliyowaamuru Israeli.[#Neh 3:26; 12:37; Ezr 7:6; Isa 8:20; Yer 8:8,9; 2 Nya 34:15; Mal 4:4]
2Naye Ezra, kuhani, akaileta Torati mbele ya mkutano mzima, wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza na mwezi wa saba.[#Kum 31:11,12; 1 Pet 3:7; Law 23:24]
3Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakasikiliza kitabu cha Torati.
4Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameitengeneza kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kulia; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu.
5Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama;[#Amu 3:20]
6Ezra akamhimidi BWANA, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainamisha vichwa vyao, wakamsujudu BWANA kifudifudi.[#Hes 5:22; Neh 5:13; Mt 6:13; 1 Kor 14:16; Omb 3:41; Kut 4:31]
7Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao.[#Law 10:11]
8Nao wakasoma katika kitabu, katika Torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa.[#Hab 2:2; Mdo 8:30-35]
9Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa BWANA, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati.[#Ezr 2:63; Neh 7:65; 2 Nya 35:3; Hos 4:6; Law 23:24; Kum 16:14; Mhu 3:4; Mal 2:13; #8:9 Tazama Neh 7:65,70.]
10Kisha akawaambia, Nendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyekuwa na kitu; maana siku hii ni takatifu kwa BWANA wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya BWANA ni nguvu zenu.[#Est 9:19; Lk 11:41; Ufu 11:10]
11Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike.
12Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa.
13Hata siku ya pili wakuu wa mbari za mababu za watu wote, na makuhani, na Walawi, wakamkusanyikia Ezra, mwandishi, ili wapate kujifunza maneno ya torati.
14Wakaona ya kuwa imeandikwa katika torati, jinsi BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa, ya kwamba wana wa Israeli wakae katika vibanda, katika sikukuu ya mwezi wa saba;[#Mwa 33:17; Law 23:34]
15na ya kwamba wahubiri na kutangaza katika miji yao yote, na katika Yerusalemu, kusema, Nendeni mlimani, mkalete matawi ya mzeituni, na matawi ya mzeituni mwitu, na matawi ya mihadasi, na matawi ya mitende, na matawi ya miti minene, ili kufanya vibanda, kama ilivyoandikwa.
16Basi watu wote wakatoka, wakayaleta, wakajitengenezea vibanda, kila mtu juu ya dari la nyumba yake, na katika nyua zao, na katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja wa lango la maji, na katika uwanja wa lango la Efraimu.[#Kum 22:8; Neh 3:26; 12:39]
17Na mkutano wote wa watu, waliorudi kutoka nchi ya uhamisho wao, wakatengeneza vibanda, wakakaa katika vibanda hivyo; maana tangu siku za Yoshua, mwana wa Nuni, hadi siku ile, wana wa Israeli hawakufanya hivyo. Pakawa na furaha kubwa sana.
18Tena siku baada ya siku, tangu siku ya kwanza hadi siku ya mwisho, akasoma katika kitabu cha Torati ya Mungu. Wakafanya sikukuu muda wa siku saba; na siku ya nane palikuwa na kusanyiko la makini, kama ilivyoagizwa.[#Kum 31:10; Hes 29:35]