Nehemia 9

Nehemia 9

Taifa laungama dhambi

1Hata siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Israeli wakawa wamekusanyika, wakifunga, wenye kuvaa magunia, na kujitia udongo vichwani.[#Neh 8:2; Yos 7:6; 1 Sam 4:12; 2 Sam 1:2; Ayu 2:12; #9:1 Au ‘juu yao’.]

2Waliokuwa wa wazao wa Israeli wakajitenga na wageni wote, wakasimama, wakaziungama dhambi zao, na maovu ya baba zao.[#Ezr 10:11; Neh 13:3; Mit 28:13; Yer 3:13; 1 Yoh 1:7-9]

3Basi wakasimama mahali pao, wakasoma katika kitabu cha Torati ya BWANA, Mungu wao, muda wa robo ya siku; na robo nyingine wakaungama na kumwabudu BWANA, Mungu wao.[#Neh 8:7]

4Ndipo wakasimama katika jukwaa la Walawi, Yeshua, na Bani, na Kadmieli, na Shebania, na Buni, na Sherebia, na Bani, na Kenani, wakamlilia BWANA, Mungu wao, kwa sauti kuu.

5Ndipo Walawi, Yeshua na Kadmieli, na Bani, na Hashabneya, na Sherebia, na Hodia, na Shebania, na Pethahia, wakasema, Simameni, mkamhimidi BWANA, Mungu wenu, tangu milele na hata milele. Na lihimidiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.[#Kut 15:6,11; 1 Nya 29:13; 2 Kor 4:6]

6Ezra akasema, Wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako; wewe ulifanya mbingu, mbingu za mbingu, pamoja na jeshi lake lote, dunia na vyote vilivyomo, bahari na vitu vyote vilivyomo, nawe unavihifadhi vitu hivi vyote; na jeshi la mbinguni lakusujudu wewe.[#Kum 6:4; Isa 37:16; Mk 12:29; Ufu 14:7; Kum 10:14; Zab 36:6; #9:6 Makala ya Kiebrania haina maneno haya.]

7Wewe ndiwe BWANA, Mungu, uliyemchagua Abramu, na kumtoa katika Uri wa Wakaldayo, na kumpa jina la Abrahamu;[#Mwa 11:31]

8nawe ukauona moyo wake kuwa mwaminifu mbele zako, ukafanya agano naye, kumpa nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Myebusi, na Mgirgashi, naam, kuwapa wazao wake; nawe umetimiza ahadi yako kwani u mwenye haki.[#Yos 23:14]

9Tena uliyaona mateso ya baba zetu katika Misri, ukakisikia kilio chao, huko kando ya Bahari ya Shamu;[#9:9 Au Bahari ya Mafunjo.]

10nawe ukaonesha ishara nyingi na mambo ya maajabu juu ya Farao, watumishi wake wote, na watu wote wa nchi yake; kwa maana ulijua ya kuwa waliwatenda kwa kutakabari; ukajipatia jina linalodumu hata leo.[#Kut 9:16; Yer 32:20; Dan 9:15; Rum 9:17]

11Nawe uliipasua bahari mbele yao, hata wakapita katikati ya bahari katika nchi kavu; na wale waliokuwa wakiwafuatia ukawatupa vilindini, kama jiwe katika maji makuu.

12Zaidi ya hayo ukawaongoza kwa nguzo ya wingu mchana; na kwa nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea.[#Kut 13:21]

13Tena ulishuka juu ya mlima Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki, na sheria za kweli, na amri nzuri na maagizo;[#Zab 19:8,9; Rum 7:12]

14ukawajulisha sabato yako takatifu, na ukawapa maagizo, na amri, na sheria, kwa mkono wa mtumishi wako, Musa.[#Mwa 2:3; Kut 20:8; Isa 56:2; Mk 2:27; Ebr 4:9]

15Ukawapa chakula toka mbinguni, kwa ajili ya njaa yao, na kwa ajili yao ukaleta maji kutoka mwambani, kwa sababu ya kiu yao, ukawaamuru waingie na kuimiliki, nchi ambayo umeinua mkono wako kuwapa.[#Kut 16:14,15; Yn 6:31; Kum 1:8]

16Lakini wao na baba zetu wakatakabari, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wala hawakuzisikiliza amri zako,[#Kum 31:27; 2 Nya 30:8; Zab 106:6; Yer 19:15]

17ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.[#Zab 78:11; Hes 14:4; Kut 34:6; Hes 14:18; Zab 86:5,15; Yoe 2:13]

18Naam, hata walipojifanyia ndama ya kusubu, na kusema, Huyu ndiye Mungu wako aliyekupandisha kutoka Misri, tena walipokuwa wamefanya machukizo makuu;

19hata hivyo wewe kwa wingi wa rehema zako hukuwaacha jangwani; nguzo ya wingu haikuondoka kwao wakati wa mchana, ili kuwaongoza njiani; wala nguzo ya moto haikuondoka wakati wa usiku, ili kuwapa mwanga na kuwaonesha njia watakayoiendea.[#Zab 106:45; Kut 13:21,22; Hes 14:14]

20Ukawapa na roho yako mwema ili kuwaelimisha, wala hukuwanyima mana vinywani mwao, tena ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.[#Hes 11:17; Isa 63:11]

21Naam, muda wa miaka arubaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba.[#Kum 8:4; Zab 34:10]

22Pamoja na hayo ukawapa falme na taifa za watu, ulizowagawia sawasawa na mafungu yao; hivyo wakaimiliki nchi ya Sihoni, naam, nchi yake mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu, mfalme wa Bashani.

23Watoto wao nao uliwaongeza kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi ile, uliyowaambia baba zao kuwa wataingia kuimiliki.[#Mwa 15:5; 1 Nya 27:23]

24Basi wale watoto wakaingia wakaimiliki nchi, nawe ukawatiisha wenyeji wa nchi mbele yao, ndio Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, na watu wa nchi, wawatende kama wapendavyo.

25Wakaitwaa miji yenye ngome, na nchi yenye utajiri, wakazitamalaki nyumba zilizojaa vitu vyema, visima vilivyochimbwa, mizabibu, na mizeituni, na miti mingi yenye matunda; hivyo wakala, wakashiba, wakanenepa, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.[#Kum 8:7-10; Eze 20:6; Kum 6:11; 32:15; Hos 13:6; 1 Fal 8:66; Rum 2:4]

26Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako waliowaonya ili wapate kukurudia wewe; wakakufuru sana.[#Mt 21:35; Mdo 7:52]

27Kwa sababu hiyo ukawatia katika mikono ya adui zao, waliowasumbua; na wakati wa shida yao, walipokulilia, uliwasikia kutoka mbinguni; na kwa wingi wa rehema zako ukawapa waokozi waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.

28Lakini walipokuwa wamekwisha kustarehe, walitenda mabaya tena mbele zako; kwa hiyo ukawaacha katika mikono ya adui zao, nao wakawatawala; hata hivyo waliporejea na kukulilia, uliwasikia toka mbinguni; ukawaokoa mara nyingi kwa rehema zako;

29ukawashuhudia ili uwarudishe tena katika sheria yako; lakini walitakabari, wasizisikilize amri zako, bali wakayaasi maagizo yako, (ambazo mtu akizitenda ataishi katika hizo), nao wakayaondoa mabega yao, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wasitake kusikiliza.[#Kum 4:26; Yer 25:3-7; Hos 6:5; Law 18:5; Mt 19:17; Lk 10:28; Rum 10:5; Gal 3:12]

30Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako; wao wasitake kusikiliza; kwa hiyo ukawatia katika mikono ya watu wa nchi.[#Zab 78:8,40; Isa 63:10; Yer 7:25; Mdo 7:51]

31Ila kwa rehema zako nyingi hukuwakomesha kabisa, wala kuwaacha; kwa maana wewe u Mungu mwenye neema na rehema.[#Yer 5:10]

32Basi sasa, Ee Mungu, mkuu, mwenye uweza, Mungu wa kuogofya, mwenye kushika maagano na rehema, mashaka yote yaliyotupata sisi, wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na manabii wetu, na baba zetu, na watu wako wote, tangu zamani za wafalme wa Ashuru hata leo, na yasihesabiwe kuwa ni madogo.[#2 Fal 17:3; Isa 7:17,18]

33Lakini wewe u mwenye haki, katika hayo yote yaliyotupata; maana wewe umetenda yaliyo kweli, lakini sisi tumetenda yaliyo maovu;[#Mwa 18:25; Zab 119:137; Dan 9:14]

34na wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na baba zetu, hawakuishika sheria yako, wala hawakuzisikiliza amri zako na shuhuda zako, ulizowashuhudia.

35Kwa kuwa hawakukutumikia wewe katika ufalme wao, na katika wema wako mkuu uliowapa, na katika nchi ile kubwa yenye neema uliyowapa mbele yao, wala hawakubadili nia na kuyaacha mabaya yao.

36Tazama, sisi hapa tu watumwa leo, na katika nchi hii uliyowapa baba zetu, wapate kula matunda yake na mema yake, tazama, sisi hapa tu watumwa ndani yake.[#Kum 28:48]

37Nayo yawapatia faida nyingi wafalme uliowaweka kututawala kwa sababu ya dhambi zetu; tena wana mamlaka juu ya miili yetu, na juu ya wanyama wetu, kadiri wapendavyo, nasi tuko katika dhiki kuu.[#Kum 28:33,48]

Waliolitia Agano mhuri

38Na kwa sababu ya hayo yote sisi tunafanya agano la hakika, na kuliandika; na wakuu wetu, na Walawi wetu, na makuhani wetu, wanalitilia mhuri.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya