Hesabu 13

Hesabu 13

Wapelelezi watumwa Kanaani

1Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia,

2Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila la baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao.[#Hes 3:2,8; Kum 1:22; 9:23]

3Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na BWANA; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli.

4Na majina yao ni haya; katika kabila la Reubeni, Shamua mwana Zakuri.

5Katika kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori.

6Katika kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune.[#Hes 14:6,30; 26:65; 34:19; Yos 14:6]

7Katika kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu.

8Katika kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni

9Katika kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu.

10Katika kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi.

11Katika kabila la Yusufu, yaani, katika kabila la Manase, Gadi mwana wa Susi.

12Katika kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali.

13Katika kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli.

14Katika kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi.

15Katika kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki.

16Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua.[#Kut 17:9; Mdo 7:45; Ebr 4:8]

17Musa akawatuma ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani,[#Mwa 14:10; Kum 1:19; Amu 1:9,19]

18mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kama ni wenye nguvu au dhaifu, kama ni wengi au wachache;

19na nchi wanayoikaa kama ni nzuri au mbaya na kama wanakaa katika kambi au katika ngome;

20nayo nchi ni ya namna gani, kama ni nchi ya utajiri au ya umaskini; kama ina misitu au haina. Kuweni na mioyo ujasiri, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza.[#Kum 8:7,8; Neh 9:25-35; Eze 20:6; 34:14; Kum 31:6; Yos 1:6,9; Ebr 13:6]

21Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, mpaka kuingia Hamathi.

22Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri.[#Amu 1:10; Zab 78:12]

23Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini.

24Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli.[#13:24 Maana yake ni ‘shada’.]

Taarifa ya wapelelezi

25Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arubaini.

26Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonesha matunda ya nchi.

27Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, kwa hakika, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, uthibitisho, haya ndiyo matunda yake.[#Kut 3:8; 13:5; 33:3; Kum 1:25]

28Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni wenye nguvu, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko.[#Kum 1:28; 9:1,2]

29Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.[#Kut 17:8; Amu 6:3; Hes 14:43; 1 Sam 14:48; 15:3; 30:1]

30Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara moja tukaimiliki; maana twaweza kushinda bila shaka.[#Yos 14:7; Zab 60:12; 118:10; Isa 11:10; Rum 8:31; Flp 4:13; Ebr 11:33,34]

31Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi.

32Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala wakazi wake; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu wakubwa mno.[#Mt 23:13; Amo 2:9]

33Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.[#Mwa 6:4; 1 Sam 17:4-7; Isa 40:22]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya