The chat will start when you send the first message.
1Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa BWANA;
Kama mifereji ya maji huugeuza popote apendapo.
2Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe;[#1 Sam 16:7; Yer 17:10; Yn 2:24]
Bali BWANA huipima mioyo.
3Kutenda haki na hukumu[#Hos 6:6]
Humpendeza BWANA kuliko kutoa sadaka.
4Mwenye kiburi na moyo wa majivuno,[#Mit 24:20]
Taa yake ni dhambi.
5Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu;
Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.
6Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo
Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti.
7Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali;
Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu.
8Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana;
Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa.
9Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini,
Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.
10Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu;[#Yak 4:5]
Jirani yake hapati fadhili machoni pake.
11Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima;
Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa.
12Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya;[#1 Kor 10:10; Rum 2:8]
Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia.
13Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini,[#Zab 58:4; Zek 7:11; Mdo 7:57; Mt 7:2]
Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.
14Kipawa cha siri hutuliza hasira;
Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali.
15Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu;
Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu.
16Mtu aikosaye njia ya busara
Atakaa katika mkutano wao waliokufa.
17Mtu apendaye anasa atakuwa maskini;
Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.
18Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki;[#Isa 43:3,4]
Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili.
19Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika;
Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.
20Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima;[#Zab 112:3; Mit 10:22; Mt 25:3]
Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza.
21Aandamaye haki na fadhili,[#1 Kor 15:58]
Ataona uhai na haki na heshima.
22Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu;
Na kuziangusha nguvu za tumaini lao.
23Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake,
Atajilinda nafsi yake na taabu.
24Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi;
Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake.
25Matakwa yake mtu mvivu humwua,
Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi.
26Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa;
Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi.
27Sadaka ya wasio haki ni chukizo;
Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!
28Shahidi wa uongo atapotea;
Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo.
29Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu;
Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake.
30Hapana hekima, wala ufahamu,
Wala shauri, juu ya BWANA.
31Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita;
Lakini BWANA ndiye aletaye wokovu.