Mithali 24

Mithali 24

1Usiwawaonee wivu watu waovu,

Wala usitamani kuwa pamoja nao;

2Kwa maana moyo wao hufikiri dhuluma,

Na midomo yao huongea madhara.

3Nyumba hujengwa kwa hekima,

Na kwa ufahamu huthibitika,

4Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa

Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.

5Mtu mwenye hekima ana nguvu;

Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo;

6Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita;

Na kwa wingi wa washauri huja wokovu.

7Kwa mpumbavu hekima haipatikani;

Hafumbui kinywa chake langoni.

8Mtu afikiriye kutenda maovu,

Watu watamwita mtundu;

9Fikira za mpumbavu ni dhambi,[#Mwa 6:5; Zab 119:113; Mt 9:4; Mdo 8:22; 2 Kor 10:5]

Na mwenye mzaha huwachukiza watu.

10Ukizimia siku ya taabu,

Nguvu zako ni chache.

11Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe;[#Isa 58:6,7; 1 Yoh 3:16]

Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe.

12Ukisema, Sisi hatukujua hayo;[#Ayu 34:11; Yer 32:19; Rum 2:6; Ufu 2:23]

Je! Yeye aipimaye mioyo siye afahamuye?

Naye ailindaye nafsi yako siye ajuaye?

Je! Hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake?

13Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema,

Na sega la asali lililo tamu ulionjapo.

14Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako;

Ikiwa umekwisha kuiona;

Ndipo itakapofuata thawabu;

Wala tumaini lako halitabatilika.

15Ewe mtu mbaya, usiyavizie makao yake mwenye haki;

Wala usipaharibu mahali pake pa kupumzika;

16Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena;[#Zab 34:19; Mik 7:8]

Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.

17Usifurahi, adui yako aangukapo;

Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

18BWANA asije akaliona hilo, likamkasirisha;

Akageuzia mbali naye hasira yake.

19Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya;

Wala usiwahusudu wabaya;

20Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu;[#Zab 11:6; Isa 3:11]

Taa ya mtu mbaya itazimika.

21Mwanangu, mche BWANA, na mfalme;[#Rum 13:7; 1 Pet 2:17]

Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;

22Maana msiba wao utatokea kwa ghafla;

Tena ni nani aujuaye uharibifu wa miaka yao.

Maneno mengine ya wenye hekima

23Haya nayo pia ni maneno ya wenye akili.[#Kum 1:17; 2 Nya 19:7; Mit 18:5; Yn 7:24]

Kupendelea watu katika hukumu si kwema.

24Amwambiaye mtu mwovu, Wewe una haki;[#Isa 5:23]

Makabila ya watu watamlaani, taifa watamchukia.

25Bali kwao wakemeao furaha itakuwako;

Na baraka ya kufanikiwa itawajilia.

26Aibusu midomo atoaye jawabu la haki.

27Tengeneza kazi yako huko nje,

Jifanyizie kazi yako tayari shambani,

Ukiisha, jenga nyumba yako.

28Usimshuhudie jirani yako pasipo sababu,[#Efe 4:25]

Wala usidanganye kwa midomo yako.

29Usiseme, Nitamtenda kama alivyonitenda mimi;[#Mt 5:39]

Nitamlipa mtu huyo sawasawa na tendo lake.

30Nilipita karibu na shamba la mvivu,

Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.

31Kumbe! Lote pia limemea miiba;[#Yer 4:3; Mt 13:7,22; Ebr 6:8]

Uso wake ulifunikwa kwa viwawi;

Na ukuta wake wa mawe umebomoka.

32Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana;

Niliona, nikapata mafundisho.

33Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,[#Mit 6:10-11]

Bado kukunja mikono upate usingizi!

34Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang'anyi,

Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya