The chat will start when you send the first message.
1Naingia bustanini mwangu, dada yangu, bibi arusi,[#Wim 4:16; Lk 15:7; Yn 3:29]
Nachuma manemane yangu na rihani,
Nala sega la asali na asali yangu,
Nanywa divai yangu na maziwa.
Kaleni, rafiki zangu, kanyweni,
Naam, nyweni sana, wapendwa wangu.
2Nilikuwa nimelala, lakini moyo wangu uko macho,[#Mit 8:4; Ufu 3:20]
Sikiliza! Mpendwa wangu anabisha!
Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu,
Hua wangu, mkamilifu wangu,
Kwa maana kichwa changu kimelowa umande,
Nywele zangu zina manyunyu ya usiku.
3Nimeivua kanzu yangu; niivaeje?
Nimenawa miguu; niichafueje?
4Mpendwa wangu aliutia mkono wake tunduni,
Na moyo wangu ukasisimuka kwa ajili yake.
5Nikaondoka nimfungulie mpendwa wangu;
Mikono yangu ilidondosha manemane,
Na vidole vyangu matone ya manemane,
Penye vipini vya komeo.
6Nilimfungulia mpendwa wangu,[#Hes 5:15; Omb 3:8]
Lakini mpendwa wangu amegeuka amepita;
(Nimezimia nafsi yangu aliponena),
Nikamtafuta, nisimpate,
Nikamwita, asiniitikie.
7Walinzi wazungukao mjini waliniona,[#Wim 3:3; Mdo 20:29,30]
Wakanipiga na kunitia jeraha,
Walinzi walindao kuta zake
Wakaninyang'anya shela yangu.
8Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,
Ninyi mkimwona mpendwa wangu,
Ni nini mtakayomwambia?
Ya kwamba nazimia kwa mapenzi.
9Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako,
Wewe uliye mzuri katika wanawake,
Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako,
Hata wewe utusihi hivyo?
10Mpendwa wangu ni mweupe, tena mwekundu,
Mashuhuri miongoni mwa elfu kumi;
11Kichwa chake ni kama dhahabu safi sana,
Nywele zake ni za ukoka, nyeusi kama kunguru;
12Macho yake ni kama hua penye vijito,[#Wim 1:15]
Wakioga kwa maziwa, wakiikalia mito iliyojaa;
13Mashavu yake ni kama matuta ya rihani
Ambayo hufanyizwa manukato;
Midomo yake ni kama nyinyoro,
Inadondosha matone ya manemane;
14Mikono yake ni kama mianzi ya dhahabu,
lliyopambwa kwa zabarajadi;
Kiwiliwili chake kama kazi ya pembe,
Iliyonakishiwa kwa yakuti samawi;
15Miguu yake ni kama nguzo za marimari,
Zilizowekwa juu ya misingi ya dhahabu;
Sura yake ni kama Lebanoni,
Ni bora mfano wa mierezi;
16Kinywa chake kimejaa maneno matamu,[#Zab 45:2; Yer 31:3; Rum 8:35; Flp 3:8]
Ndiye mzuri sana kwa ujumla.
Ni huyu mpendwa wangu, ni huyu rafiki yangu,
Enyi binti za Yerusalemu.