Tobiti 14

Tobiti 14

Tobiti atoa mawaidha ya mwisho

1Basi Tobiti akaisha kushukuru.

2Na wakati alipopofuka macho umri wake amepata miaka hamsini na minane. Na baada ya miaka minane akajaliwa kuona tena; akatoa sadaka, akazidi kumcha Mungu na kumshukuru.

3Basi akazidi sana kuwa mzee; akamwita mwanawe, na watoto sita wa mwanawe, akamwambia, Mwanangu, uwatwae wanao; tazama, mimi ni mzee, nami ni tayari kuifariki dunia.

4Basi, mwanangu, uende Umedi; kwa maana nasadiki kabisa maneno yote yaliyonenwa na nabii juu ya Ninawi, ya kama utaangamizwa; bali kwa muda kutakuwako amani huko Umedi. Ndugu zetu watatawanyika duniani kutoka ile nchi nzuri, na Yerusalemu utakuwa ukiwa; na nyumba ya Mungu ndani yake itateketezwa, na kuwa ukiwa kwa muda.[#Neh 1:2—3:19]

5Hatimaye Mungu atawarehemu tena, na kuwarudisha katika nchi nao wataijenga nyumba, walakini si kama ile ya kwanza, hata majira ya zamani zile yatakapotimia. Kisha watarudi kutoka mahali walimofungwa; wataujenga Yerusalemu kwa heshima; nayo nyumba ya Mungu itajengwa ndani yake milele kwa jengo la utukufu; kama vile walivyoitabiria manabii.

6Na mataifa yote watageuka kumcha BWANA Mungu kwa kweli; nao watazizika sanamu zao.

7Na mataifa yote watamhimidi BWANA; na watu wake watamshukuru Mungu. Naye BWANA atawakuza watu wake; nao wote wampendao BWANA Mungu kwa kweli na kwa haki watafurahi, kwa kuwa amewarehemu ndugu zetu.

8Lakini wewe uishike torati na maagizo, ujioneshe kuwa mpenda sadaka na haki, ili ufanikiwe.

9Na sasa, mwanangu, uondoke kutoka Ninawi; kwa maana mambo yale aliyoyanena nabii hakika yatatokea.

10Mimi unizike kwa heshima, na mama yako pamoja nami; wala msizidi kukaa hapa Ninawi. Mwanangu, kumbuka Amani alivyomtenda Akiakaro aliyemlea; jinsi alivyomtoa kwenye nuru na kumleta kwenye giza, na jinsi alivyomlipa; lakini Akiakaro aliokoka, bali yule alipata malipo yake, maana yeye alishuka kwenye giza. Naye Manase alitoa sadaka, akaokoka katika tanzi la mauti ambalo kwamba amemtegea; bali Amani aliingia tanzini akaangamia.

Kifo cha Tobiti na Ana

11Kwa hiyo, mwanangu, fikiri hayo iyatendayo sadaka, na jinsi haki iokoavyo. Naye alipokuwa katika kusema maneno hayo, akatoa roho pale kitandani; na umri wake amepata miaka mia moja hamsini na minane. Wakamzika kwa heshima nyingi.

12Na Ana alipokufa, mwanawe akamzika pamoja na baba yake. Lakini Tobia aliondoka, pamoja na mkewe na watoto wake, kwenda Ekbatana kwa mkwewe Ragueli.

13Huko alipata kuwa mzee mwenye heshima; akawazika wakweze kwa heshima nyingi; akazirithi mali zao, na zile za Tobiti baba yake.

14Akafa huko Ekbatana, mji wa Umedi, mwenye umri wa miaka mia moja ishirini na saba.

15Lakini kabla hajafa akapata habari za kuangamizwa Ninawi, ambao ulitekwa na Nebukadreza na Ahasuero; na kabla ya kufa kwake alipata kusimanga juu ya Ninawi. Ndio mwisho.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya