Hekima ya Sulemani 4

Hekima ya Sulemani 4

1Yaani, utakatifu, kumbukumbu lake ladumu milele, ambao hukubalika mbele za Mungu na wanadamu;[#Sira 16:3]

2ukiwapo, watu huuiga; ukiwa umeondoka, watu huutamani; siku zote za milele unaendelea umevikwa taji la kushinda, umeshinda katika mashindano ya tuzo zisizo na janaba.

3Bali uzao uzidio wa wasio haki hauleti faida, wala kwa wana wa haramu hawatatia mizizi, wala kushikisha miche imara.

4Kwa kuwa iwapo imetoa matawi na kufanikiwa kwa muda kitambo, hata hivyo itatikiswa kwa upepo, na kwa nguvu za dhoruba itang'olewa.

5Nayo matawi hayo yatavunjika yasijekomaa, matunda yatakuwa hayafai, yasiyoiva kamwe, hafifu.

6Maana watoto waliozaliwa isivyo halali huwashuhudia wazazi wao uovu wao, hapo Mungu atakapowachunguza.

Kifo cha mwadilifu kabla ya wakati

7Walakini mwenye haki, ingawa amekufa kabla ya wakati wake, atastarehe.

8Kwa maana uzee ulio na heshima, siyo kama kitu chake ni wingi wa wakati tu, wala kipimo chake idadi ya miaka;

9bali ufahamu ni kama mvi kwao wanadamu, na maisha safi ni kama uzee ulio mtimilifu.

10Huyo alionekana amempendeza Mungu, akapendwa naye, hata pindi alipokaa katikati ya wakosaji akachukuliwa.[#Mwa 5:21-24; Sira 44:16; Ebr 11:5]

11Naye akahamishwa ili uovu usimgeuzie nia yake, wala hila isimdanganye roho yake;

12mradi usihiri wa utukufu hufumba yaliyo mazuri, na uvuruvuru wa tamaa hupotosha akili zilizo nyofu.

13Huyo alikamilika katika siku chache, akatimiza miaka mingi;

14na kwa kuwa roho yake ilimpendeza BWANA, akafanya haraka ya kuondoka katikati ya uovu. Lakini kwa habari ya waovu, hao huona lakini hawafahamu, wala hawatii mioyoni mwao neno hili,

15ya kwamba neema na rehema zina wateule wake, naye huwaangalia watakatifu wake.

Ushindi wa wenye haki

16Mwenye haki aliyefariki dunia

Atawahukumu wasio haki walio hai,

Na ujana uliokamilika upesi

Miaka mingi ya mzee aliye dhalimu.

17Kwa maana wasio haki watauona mwisho wake mwenye hekima, lakini hawatafahamu makusudi ya BWANA juu yake, wala kwa sababu gani alimweka salama.

18Hivyo wataona na kudhihaki, lakini BWANA atawacheka.

19Hata na baadaye watakuwa kama maiti iliyotiwa fedheha, na lawama miongoni mwa wafu milele. Yeye atawatupa chini hali ya kutekewa, atawatikisa mpaka misingi, nao wataharibika ukiwa, wataona uchungu, na kumbukumbu lao litapotea.

Hukumu ya mwisho

20Wao watatokea kwa hofu na woga, watakapohesabiwa dhambi zao; na mbele ya nyuso zao matendo yao yasiyo haki yatawatia hatiani.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya