The chat will start when you send the first message.
1Hekima huenea kwa nguvu nyingi toka pembe hii hata pembe hii ya dunia, na kuyaratibisha mambo yote kwa jinsi ya kufaa.
2Ndiyo niliyoipenda tangu ujana wangu na kuitafutatafuta, nikatamani kujichukulia hiyo mithili ya bibi arusi, nikawa na shauku ya uzuri wake.[#Sira 15:2]
3Huona fahari juu ya ungwana wake, kwa sababu hupewa kukaa na Mungu, naye BWANA, Mfalme wa wote, ameipenda.
4Mradi hufunuliwa maarifa ya Mungu, kumchagulia matendo yake.[#Mit 8:27-30]
5Hata ikiwa mali ni kitu cha kutamaniwa katika maisha haya, utajiri ni nini kuliko Hekima, iendeshayo mambo yote?
6Na ikiwa busara ndiyo itendayo kazi, nani aliye fundi wa kazi zote zilizopo kupita Hekima?
7Kama mtu akipenda haki, basi matunda ya kazi ya Hekima ni adabu; maana huwafundisha watu kiasi, na ufahamu, na haki, na ushujaa; wala hakuna mambo ya kuwafaa zaidi kwa maisha.
8Na hata mtu akiwa anatamani kuelewa na maarifa mengi ya malimwengu, Hekima hujua mambo ya kale, na kutambua mambo yajao; Hufahamu maneno ya fumbo, na kufumbua vitendawili; hutangulia kutambua ishara na maajabu, na matokeo ya majira na nyakati.
9Basi nilikusudia kujichukulia hiyo ikae nami, nikijua ya kwamba itaniletea mawazo mema kwa mashauri yake, na faraja nzuri wakati wa masumbufu na huzuni.
10Kwa ajili yake nitatukuzwa katika makutano, na kuheshimiwa machoni pa wazee ingawa ni kijana.
11Nitaonekana kuwa mwelekevu nitoapo hukumu, na mbele ya wafalme nitapewa staha.
12Nikinyamaa, wataningojea; nikiifumbua midomo yangu, watanisikiliza; nikiongeza kunena, watautia mkono kinywani.
13Kwa ajili yake nitajaliwa kupata sifa ya milele, na kuwaachia wanifuatao kumbukumbu la daima.
14Nitatawala watu, na mataifa watatumikishwa chini yangu.
15Wafalme wa kutisha wataniogopa kwa kusikia habari zangu; na miongoni mwa watu wangu nitajionesha kuwa mtawala stadi na hodari wa vita.
16Niingiapo nyumbani mwangu nitastarehe pamoja nayo; yaani, kuzungumza nayo si uchungu wala kukaa nayo si hofu; bali ni furaha na changamko.
17Basi nilitafakari mambo hayo, nikafikiri moyoni mwangu ya kama kutokuharibika kunahusiana na Hekima,
18na urafiki wake unao ukunjufu wa moyo, na kazi za mikono yake zaleta mali isiyopungua, na kuzungumza nayo kwa bidii ni ufahamu, na kupatana na maneno yake huongeza heshima; hivyo nilizunguka nikitafuta-tafuta jinsi ya kujichukulia hiyo.
19Nami nilikuwa mtoto mwenye adabu, nikajaliwa roho mwema;
20walakini afadhali tuseme, nikiwa mwema, niliingia katika mwili mzuri;
21lakini nilitambua ya kwamba siwezi kuwa na Hekima, nisipopewa na Mungu; naam, tena, hata kujua ni nani atoaye neema ni kazi ya ufahamu; basi, nilimwomba BWANA na kumsihi; na kwa moyo wangu wote nilimwambia: