The chat will start when you send the first message.
1BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda;[#Kut 35:30; 1 Nya 2:20]
3nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,[#Kut 35:31; 1 Fal 7:14; Isa 28:26; 1 Kor 12:4-8]
4ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba,
5na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.
6Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza;[#Kut 35:34; 28:3; 36:1]
7yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema;[#Kut 36:8]
8na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba;
9na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake;
10na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani;
11na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.
12BWANA akasema na Musa, na kumwambia,
13Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.[#Law 19:3; 26:2; Eze 20:12; 44:24]
14Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.[#Neh 9:14; Kum 5:12; Isa 56:6; 58:13; Eze 20:12; Kut 35:2; Hes 15:35]
15Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa.[#Mwa 2:2; Kut 16:23; 20:8-11; 23:12; 28:36; 34:21; 35:2; Law 23:3; Kum 5:12-14]
16Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.
17Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita BWANA alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika.[#Kut 20:11; Eze 20:12; Mwa 1:31]
18Hapo BWANA alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.[#Kut 24:12; 32:15; 34:28,29; Kum 4:13; 5:22; 9:10,11; 2 Kor 3:3]