Hos 2

Hos 2

1Waambieni ndugu zenu wanaume, Ami na ndugu zenu wanawake, Ruhama.[#2:1 maana yake ni Watu wangu.; #2:1 maana yake ni Aliyehurumiwa.]

Uzinzi, Adhabu na Ukombozi wa Israeli

2Msihini mama yenu, msihini; kwa maana yeye si mke wangu, wala mimi si mume wake; na ayawekee mbali mambo ya uasherati wake yasiwe mbele ya uso wake, na mambo ya uzinzi wake yasiwe kati ya maziwa yake;[#Isa 50:1; Yer 3:1,9,13; Eze 16:25; Hos 1:2]

3nisije nikamvua nguo zake akawa uchi, nikamweka katika hali aliyokuwa nayo siku ya kuzaliwa kwake, na kumfanya kama jangwa, na kumweka kama nchi kame, na kumfisha kwa kiu;[#Yer 13:22; Eze 19:13; Amo 8:11]

4naam, sitawaonea rehema watoto wake; kwa maana ni watoto wa uzinzi.

5Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu.[#Yer 44:17]

6Basi kwa ajili ya hayo, angalia, nitaiziba njia yako kwa miiba, nami nitafanya kitalu juu yake, asipate kuyaona mapito yake.[#Ayu 19:8]

7Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa.[#Lk 15:18; Eze 16:8]

8Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye aliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali.

9Basi kwa ajili ya hayo, nitaitwaa tena ngano yangu kwa wakati wake, na divai yangu kwa wakati wake, nami nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu, vya kumfunika uchi wake.

10Na sasa nitaifunua aibu yake mbele ya macho ya wapenzi wake, wala hapana mtu atakayemwokoa katika mkono wangu.

11Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.[#Isa 24:7; Yer 7:34; Amo 8:10]

12Nami nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema, Hii ndiyo ujira wangu niliopewa na wapenzi wangu; nami nitaifanya kuwa msitu, na wanyama wa mashamba wataila.[#Isa 5:5]

13Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali, aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito asema BWANA.[#Amu 3:7; Eze 23:40]

14Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo.[#Eze 20:35]

15Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.[#Isa 65:10; Omb 3:21; Zek 9:12; 1 Kor 13:13; Yos 7:24-26]

16Tena siku hiyo itakuwa, asema BWANA, utaniita Ishi, wala hutaniita tena Baali.[#2:16 maana yake ni Mume wangu.; #2:16 maana yake ni Bwana wangu.]

17Kwa maana nitayaondoa majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao.[#Kut 23:13]

18Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini.[#Ayu 5:23; Zek 9:10; Isa 11:6; 2:4; Law 26:5; Yer 23:6]

19Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema.

20Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua BWANA.[#Isa 54:13; Yer 31:33]

21Tena itakuwa siku hiyo, mimi nitaitika, asema BWANA; nitaziitikia mbingu, nazo zitaiitikia nchi;[#Zek 8:12]

22nayo nchi itaiitikia nafaka na divai na mafuta; nayo yataiitikia Yezreeli.

23Nami nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitamrehemu yeye asiyepewa rehema; nami nitawaambia wale wasiokuwa watu wangu, Ninyi ndinyi watu wangu; nao watasema, Wewe ndiwe Mungu wangu.[#Zek 10:9; 13:9; Rum 9:25; 1 Pet 2:10]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania