Hos 9

Hos 9

Adhabu kwa ajili ya Dhambi ya Israeli

1Usifurahi, Israeli, kwa sababu ya furaha, kama hao mataifa; kwa kuwa umezini juu ya Mungu wako, umependa ujira katika kila sakafu ya nafaka.

2Sakafu na shinikizo hazitawalisha, na divai mpya itampungukia.

3Hawatakaa katika nchi ya BWANA; lakini Efraimu atarudi Misri, nao watakula chakula kinajisi katika Ashuru.[#Law 18:25; Kum 4:26,27; Hos 11:5; Eze 4:13]

4Hawatammiminia BWANA divai, wala hazitampendeza sadaka zao; mkate wao utakuwa kama chakula cha matanga kwao; wote watakaokila watatiwa unajisi; kwa maana mkate wao utakuwa kwa shauku zao; hautaingia katika nyumba ya BWANA.[#Kum 26:14]

5Mtafanya nini katika siku ya mkutano wa idi, na katika siku ya karamu ya BWANA?

6Kwa maana, tazama, wamekwenda zao ili kukimbia uharibifu, lakini Misri itawakusanya, Nofu itawazika; vitu vyao vya fedha viwapendezavyo, magugu yatavimiliki; miiba itakuwa katika hema zao.

7Siku za kupatilizwa zimekuja, siku za kulipa zimefika; Israeli atayajua hayo; huyo nabii ni mpumbavu, huyo mtu mwenye roho ana wazimu; kwa sababu ya wingi wa uovu wako, na kwa sababu uadui umekuwa mkubwa.[#Lk 21:22]

8Efraimu alikuwa mlinzi pamoja na Mungu wangu; na huyo nabii, mtego wa mwinda ndege u katika njia zake zote; katika nyumba ya Mungu wake umo uadui.

9Wamejiharibu mno, kama katika siku za Gibea; ataukumbuka uovu wao, atazilipiza dhambi zao.[#Amu 19:1-30]

10Mimi nalimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami naliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza, wakati wake wa kwanza; lakini walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda.[#Kum 32:10; Hes 25:1-5]

11Naye Efraimu, utukufu wake utarukia mbali kama ndege, uzazi hautakuwako, wala aliye na mimba, wala achukuaye mimba.

12Wajapolea watoto wao, mimi nitawanyang’anya watoto wao, asisalie hata mtu mmoja; naam, ole wao! Nitakapoondoka na kuwaacha.[#Kum 31:17; 1 Sam 28:15; Hos 5:6]

13Efraimu amepandwa mahali pazuri, kama nilivyoona Tiro; lakini Efraimu atamtolea mwuaji watoto wake.

14Wape, Ee BWANA; utawapa kitu gani? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na maziwa makavu.[#Lk 23:29]

15Uovu wao wote u katika Gilgali; maana huko naliwachukia; kwa sababu ya uovu wa matendo yao nitawafukuza watoke katika nyumba yangu; sitawapenda tena; wakuu wao wote ni waasi.

16Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana.

17Mungu wangu atawatupilia mbali, kwa sababu hawakumsikiliza; nao watakuwa watu wa kutanga-tanga kati ya mataifa.[#2 Fal 17:18]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania