The chat will start when you send the first message.
1Ikakaribia sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Sikukuu ya Pasaka.[#Mt 26:1-5; Mk 14:1,2]
2Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu.[#Lk 20:19]
3Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara.[#Mt 26:14-16; Mk 14:10,11; #Yn 13:2,27]
4Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao.
5Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha.
6Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano.
7Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka.[#Mt 26:17-29; Mk 14:12-25; #Kut 12:18-20]
8Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila.
9Wakamwambia, Wataka tuandae wapi?
10Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye.
11Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu?
12Naye atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo.
13Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.[#Lk 19:32]
14Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye.
15Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu;
16kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.[#Lk 13:29]
17Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi;
18Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja.
19Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.[#1 Kor 11:23-25; Mdo 27:35]
20Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.][#Kut 24:8; Yer 31:31; Zek 9:11]
21Walakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani,[#Yn 13:21,22]
22Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye!
23Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni yupi miongoni mwao atakayelitenda jambo hilo.
24Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa.[#Mt 18:1; Mk 9:34; Lk 9:46]
25Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili;[#Mt 20:25-27; Mk 10:42-44]
26lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye.[#Mt 23:11; Mk 9:35]
27Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.[#Yn 13:12-15]
28Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu.
29Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi;[#Lk 12:32]
30mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.[#Mt 19:28]
31Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano;[#Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Yn 13:36-38; #2 Kor 2:11; Amo 9:9]
32lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.[#Yn 17:11,15,20; Zab 51:13]
33Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni.
34Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.
35Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La![#Mt 10:9-10; Mk 6:8-9; Lk 9:3; 10:4]
36Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue.
37Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake.[#Isa 53:12; Lk 22:52]
38Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.
39Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye.[#Mt 26:30,36-46; Mk 14:26,32-42; #Lk 21:37; Yn 18:1]
40Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni.
41Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba,
42akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [[#Mt 6:10]
43Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.[#1 Fal 19:5; Yn 12:29]
44Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]
45Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni.
46Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.
47Basi alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye ni mmoja wa wale Thenashara, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu.[#Mt 26:47-56; Mk 14:43-49; Yn 18:2-11]
48Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?
49Na wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotukia, walisema, Bwana, tuwapige kwa upanga?
50Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume.
51Yesu akajibu akasema, Mwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya.
52Yesu akawaambia wakuu wa makuhani, na maakida wa hekalu, na wazee, waliokuja juu yake, Je! Mmekuja wenye panga na marungu kama kukamata mnyang’anyi?[#Lk 22:37]
53Kila siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza.[#Lk 19:47; 21:37; Yn 7:30; 8:20; Kol 1:13]
54Wakamkamata, wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali.[#Mt 26:57,58,69-75; Mk 14:53,54,66-72; Yn 18:12-18,25-27]
55Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao.
56Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye.
57Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui.
58Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi.
59Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya.
60Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika.
61Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu.[#Lk 22:34]
62Akatoka nje akalia kwa majonzi.
63Na wale watu waliokuwa wakimshika Yesu walimfanyia dhihaka, wakampiga.[#Mt 26:67,68; Mk 14:65]
64Wakamfunika macho, kisha wakamwuliza-uliza wakisema, Tabiri, ni nani aliyekupiga?
65Wakamtolea na maneno mengine mengi ya kumtukana.
66Hata kulipokucha, walikutanika jamii ya wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, wakamleta katika baraza yao, wakisema,[#Mt 26:59-66; Mk 14:55-64]
67Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie. Akawaambia, Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa.[#Yn 3:12; 8:45; 10:24]
68Tena, nikiwauliza, hamtajibu.
69Lakini tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi.[#Dan 7:13; Zab 110:1]
70Wakasema wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye.
71Wakasema, Basi, tuna haja gani tena ya ushuhuda? Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake.