The chat will start when you send the first message.
1Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana.[#Flp 2:18; 4:4]
Kuwaandikieni mambo yale yale hakuniudhi mimi, bali kutawafaa ninyi.
2Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao.[#Ufu 22:15]
3Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili.[#Rum 2:29]
4Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi.[#2 Kor 11:18,22]
5Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo,[#Mdo 23:6; 26:5; Rum 11:1; Lk 1:59; 2:21]
6kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.[#Mdo 8:3; 22:4; 26:9-11]
7Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.[#Mt 13:44,46]
8Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;
9tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani;[#Rum 3:21,22]
10ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;[#Rum 6:3-5; 8:17; Gal 6:17]
11ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu.[#Mdo 4:2; Ufu 20:5,6]
12Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu.[#1 Tim 6:12; Mdo 9:6]
13Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;
14nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.[#1 Kor 9:24]
15Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo.[#1 Kor 2:6]
16Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo.[#Gal 6:16]
17Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi.[#1 Kor 4:16; 11:1; 1 The 1:7; 1 Pet 5:3]
18Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo;[#1 Kor 1:23; Gal 6:12]
19mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani.[#Rum 16:18]
20Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;[#Efe 2:6; Kol 3:1; Ebr 12:22]
21atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.[#1 Kor 15:43,49,53]