Zab 71

Zab 71

Sala ya Ulinzi wa Daima na Msaada

1Nimekukimbilia Wewe, BWANA,

Nisiaibike milele.

2Kwa haki yako uniponye, uniopoe,

Unitegee sikio lako, uniokoe.

3Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,[#Zab 44:4]

Nitakakokwenda sikuzote.

Umeamuru niokolewe,

Ndiwe genge langu na ngome yangu.

4Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,

Katika mkono wake mwovu, mdhalimu,

5Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU,[#Yer 17:7; Rum 15:13]

Tumaini langu tokea ujana wangu.

6Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,[#Zab 22:9; Isa 46:3; Yer 3:4]

Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,

Ninakusifu Wewe daima.

7Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi,[#Isa 8:18; Zek 3:8; 1 Kor 4:9]

Na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.

8Kinywa changu kitajazwa sifa zako,

Na heshima yako mchana kutwa.

9Usinitupe wakati wa uzee,

Nguvu zangu zipungukapo usiniache.

10Kwa maana adui zangu wananiamba,[#2 Sam 17:1; Mt 27:1]

Nao wanaoniotea roho yangu hushauriana.

11Wakisema, Mungu amemwacha,

Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya.

12Ee Mungu, usiwe mbali nami;[#Zab 22:11; 35:22; 70:1]

Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.

13Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu.[#Zab 35:4; 40:14]

Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.

14Nami nitatumaini daima,

Nitazidi kuongeza sifa zake zote.

15Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako[#Zab 35:28; 40:5]

Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.

16Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU;[#Zek 10:12; Efe 3:16; Flp 4:13; 2 Tim 2:1]

Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.

17Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;

Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.

18Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi,

Ee Mungu, usiniache.

Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako,

Na kila atakayekuja uweza wako.

19Na haki yako, Ee Mungu,[#Zab 57:10; Mit 24:7; Isa 5:16; Kut 15:11; Zab 35:10; Isa 40:18,25]

Imefika juu sana.

Wewe uliyefanya mambo makuu;

Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?

20Wewe, uliyetuonyesha mateso mengi, mabaya,[#Zab 60:3; Hos 6:1]

Utatuhuisha tena.

Utatupandisha juu tena

Tokea pande za chini ya nchi.

21Laiti ungeniongezea ukuu!

Urejee tena na kunifariji moyo.

22Nami nitakushukuru kwa kinanda,[#2 Fal 19:22; Isa 60:9]

Na kweli yako, Ee Mungu wangu.

Nitakuimbia Wewe kwa kinubi,

Ee Mtakatifu wa Israeli.

23Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo,[#Zab 103:4]

Na nafsi yangu uliyoikomboa.

24Ulimi wangu nao utasimulia

Haki yako mchana kutwa.

Kwa maana wameaibishwa,

Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania