The chat will start when you send the first message.
1Maskani zako zapendeza kama nini,[#Zab 26:8; 27:4; Ebr 9:23,24; Ufu 21:2]
Ee BWANA wa majeshi!
2Nafsi yangu imezionea shauku nyua za BWANA,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai.
3Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake,
Kwenye madhabahu zako, Ee BWANA wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
4Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
5Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
6Wakipita kati ya bonde la Vilio,
Hulifanya kuwa chemchemi,
Naam, mvua ya vuli hulivika baraka
7Huendelea toka nguvu hata nguvu,[#Kum 16:16]
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
8BWANA, Mungu wa majeshi, uyasikie maombi yangu,
Ee Mungu wa Yakobo, usikilize,
9Ee Mungu, ngao yetu, uangalie,[#Mwa 15:1]
Umtazame uso masihi wako.
10Hakika siku moja katika nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu.
Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu,
Kuliko kukaa katika hema za uovu.
11Kwa kuwa BWANA, Mungu, ni jua na ngao,
BWANA atatoa neema na utukufu.
Hatawanyima kitu chema
Hao waendao kwa ukamilifu.
12Ee BWANA wa majeshi,
Heri mwanadamu anayekutumaini Wewe.