Rut 3

Rut 3

Ruthu na Boazi kwenye Uga wa Kupepetea

1Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema?[#1 Kor 7:36; 1 Tim 5:8; Kum 4:40; Rut 1:9; Zab 128:2; Yer 22:15,16]

2Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani.[#Rut 2:8]

3Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa.[#2 Sam 14:2]

4Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na yeye atakuambia utakalofanya.

5Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya.[#Efe 6:1; Kol 3:20]

6Basi akashuka mpaka ugani; akafanya yote kama vile mkwewe alivyomwagiza.

7Ikawa huyo Boazi alipokwisha kula na kunywa, na moyo wake umekunjuka, alikwenda kulala penye mwisho wa chungu ya nafaka; na huyo mwanamke akaja taratibu, akaifunua miguu yake, akajilaza papo hapo.[#Amu 19:6; 2 Sam 13:28; Est 1:10]

8Na ikawa usiku wa manane yule mtu akasituka, akajigeuza; na kumbe! Yupo mwanamke amelala miguuni pake.

9Akasema, Ama! Ni nani wewe? Akamjibu, Ni mimi, Ruthu, mjakazi wako; uitande nguo yako juu ya mjakazi wako; kwa kuwa ndiwe wa jamaa aliye karibu.[#Eze 16:8]

10Akamwambia, Mwanangu, ubarikiwe na BWANA; umezidi kuonyesha fadhili zako mwisho kuliko mwanzo, kwa vile usivyowafuata vijana, kama ni maskini kama ni matajiri.[#Rut 2:20; 1:8]

11Basi, mwanangu, usiogope; mimi nitakufanyia yote uyanenayo; kwa maana mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema.[#Mit 12:4; 31:10,29,31]

12Tena ndiyo kweli ya kuwa mimi ni wa jamaa yako aliye karibu; lakini kuna mtu wa jamaa aliye karibu kuliko mimi.[#Rut 2:20; 4:1; 1 The 4:6]

13Wewe ungoje usiku huu; kisha, asubuhi, kama akikubali kukufanyia impasavyo jamaa, haya, na akufanyie; lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa; BWANA aishivyo. Ulale wewe hata asubuhi.[#Kum 25:5; Rut 4:5; Mt 22:24; Amu 8:19; Yer 4:2; Ebr 6:16]

14Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hata asubuhi; akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenziwe; maana Boazi amesema, Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika penye uga.[#Rum 12:17; 14:16; 1 Kor 10:32; 2 Kor 8:21; 1 The 5:22; 1 Pet 2:12]

15Tena alisema, Lete hapa shela yako uliyoivaa, uishike; naye akaishika; naye akampimia vipimo sita vya shayiri akamtwika; kisha huyo mwanamke akaenda zake mjini.

16Basi alipofika kwa mkwewe, huyo akamwuliza, Je! Mwanangu, imekuwaje? Akamwambia yote yule mtu aliyomfanyia.

17Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu.

18Naye mkwewe akasema, Basi, mwanangu, tulia; hata utakapojua jinsi litakavyotukia jambo hili; kwa sababu mtu huyu hataridhika, asipolimaliza jambo hilo leo.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania