1 Wakorintho 9

1 Wakorintho 9

1JE! mimi si mtume? mimi si huru? sikumwona Yesu Kristo Bwana wetu? ninyi si kazi yangu katika Bwana?

2Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, illakini ni mtume kwenu ninyi; kwa maana muhuri ya utume wangu ni ninyi katika Bwana.

3Jawabu yangu kwa wale wanaoniuliza ni hii.

4Je! hatuna uwezo wa kula na kunywa?

5Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa?

6Au je! ni mimi peke yangu na Barnaba tusio na uwezo kutokufanya kazi?

7Nani aendae vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Nani apandae mizabibu asiokula baadhi ya matunda yake? Au nani achungae kundi, asiyekula haadhi ya maziwa ya kundi?

8Je! ninanena haya kama mwana Adamu? Au sharia nayo haisemi yayo hayo?

9Kwa maana katika sharia ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ngʼombe apurae nafaka. Je! Mungu aangalia mambo ya ngʼombe?

10Au anena hayo kwa ajili yetu bassi? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu kama alimae nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini; nae apurae nafaka kwa matumaini ni haki yake kupata sehemu ya matumaini yake.

11Ikiwa sisi twaliwapandieni vitu vya rohoni, je! ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?

12Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huu; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Injili ya Kristo.

13Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula sehemu ya vitu vya hekalu, na wale waikhudumiao madhbahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhbahu?

14Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waikhubirio Injili wamzukiwe kwa Injili.

15Lakini sikutumia mambo haya hatta moja. Wala sikuvaandika haya illi iwe hivyo kwangu; maana ni kheri nife kuliko mtu aliye vote abatilishe huku kujisihi kwangu.

16Maana, ijapokuwa naikhubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimepewa sharti; tena ole wangu nisipoikhubiri.

17Maana nikiitenda kazi hii kwa khiari yangu nina thawabu; kama si kwa khiari yangu, illakini nimeaminiwa uwakili.

18Bassi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nikhubiripo, nitatoa Injili ya Kristo bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu haki yangu niliyo nayo katika Injili.

19Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, illi nipate watu wengi zaidi.

20Nalikuwa Myahudi kwa Wayahudi, illi niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sharia, nalikuwa kama chini ya sharia, illi niwapate walio chini ya sharia.

21Kwa wale wasio na sharia nalikuwa kama sina sharia. Si kana kwamba sina sharia mbele za Mungu, hali mwenye sharia mbele za Kristo, illi niwapate wasio na sharia.

22Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, illi niwapate wanyonge. Nalikuwa mtu wa hali zote kwa watu wote, illi nipate kuwaokoa watu kwa njia zote.

23Nami nafanya haya yote kwa ajili ya Injili nipate kuishiriki pamoja na wengine.

24Hamjui, ya kuwa washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeao tunzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, illi mpate.

25Na killa ashindanae hujiweza katika yote: bassi hao kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi isiyoharibika.

26Hatta mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitae; napigana vivyo hivyo, si kama apigae hewa:

27bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwakhubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania