1 Wathessaloniki 1

1 Wathessaloniki 1

1PAOLO, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathessaloniki, katika Mungu Baba, na Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

2Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu;

3wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya amani, na taabu yenu ya upendo, na uvumilivu wenu wa tumaini lililo katika Bwana Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu;

4tukijua, ndugu mnaopendwa na Mungu, uteule wenu,

5kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthubutifu mwingi; kama mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu.

6Mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea Neno katika mateso mengi pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu,

7hatta mkawa mfano kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya.

8Maana kutoka kwenu Neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu: bali na katika killa mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea, hatta hatuna haja sisi kunena lo lote.

9Maana wao wenyewe wanatangaza khabari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu, mkaziacha sanamu illi kumtumikia Mungu aliye hayi, wa kweli,

10na kumugojea Mwana wake kutoka mbinguni, ambae alimfufua katika wafu, Yesu, anaetuokoa na ghadhabu itakayokuja.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania