1 Wakorintho 14

1 Wakorintho 14

Zitumieni Karama za Roho Kulisaidia Kanisa

1Upendo uwe lengo la maisha yenu, lakini mnapaswa pia kuzitaka karama za Roho. Na itakeni sana karama ya unabii.

2Nitafafanua ni kwa nini. Wenye karama ya kusema kwa lugha zingine hawazungumzi na watu. Huzungumza na Mungu. Hakuna anayewaelewa kwa sababu huzungumza mambo ya siri kupitia Roho.

3Lakini wanaotabiri huzungumza na watu. Huwasaidia watu kuwa imara katika imani, na huwatia moyo na kuwafariji.

4Wanaosema kwa lugha hujiimarisha wao wenyewe. Lakini wanaotabiri huliimarisha kanisa lote.

5Ningependa ninyi nyote muwe na karama ya kusema kwa lugha zingine. Lakini ninachotaka zaidi ni ninyi kutabiri. Yeyote anayetabiri ni wa muhimu zaidi kuliko wale wanaosema kwa lugha zingine. Hata hivyo, ikiwa wanaweza kufasiri lugha hizo, basi kanisa linasaidiwa kutokana na kile wanachosema.

6Ndugu zangu, je, itawasaidia nikija kwenu na kusema kwa lugha zingine? Hapana, itawasaidia pale tu nitakapowaletea ufunuo mpya au maarifa fulani, unabii au mafundisho.

7Hii ni kweli hata kwa vitu visivyo na uhai vinavyotoa sauti kama filimbi na kinubi. Ikiwa muziki hauchezwi kwa ufasaha, hutaweza kujua ni wimbo gani unaopigwa.

8Na katika vita, ikiwa tarumbeta haitatoa ishara vizuri, askari hawawezi kujua kuwa ni wakati wa kujiandaa kwa mapigano.

9Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Watu hawataweza kuelewa unachosema, ikiwa utazungumza katika lugha tofauti wasiyoitambua. Utakuwa unazungumza hewani tu!

10Ni dhahiri kuwa kuna lugha nyingi ulimwenguni, na zote zina maana.

11Lakini ikiwa sielewi maana ya maneno wanayosema wengine, kwangu itakuwa sauti ya ajabu tu, na nitasikika kama ninayetoa sauti za ajabu.

12Kwa kuwa mna nia kuhusu karama za Kiroho, muwe na hamu ya kulisaidia kanisa kuwa imara.

13Hivyo wenye karama ya kusema kwa lugha waombe ili waweze kufasiri yale wanayosema.

14Ninapoomba kwa lugha zingine, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haifanyi chochote.

15Hivyo nifanye nini? Nitaomba kwa roho yangu, lakini pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho yangu, lakini pia nitaimba kwa akili yangu.

16Unaweza ukawa unamshukuru Mungu kwa roho yako. Lakini mtu mwingine ambaye haielewi lugha unayotumia hawezi kusema “Amina” kwa maombi yako ya shukrani.

17Unaweza ukawa unamshukuru Mungu katika njia nzuri, lakini isiwasaidie wengine kuwa imara.

18Ninamshukuru Mungu kwamba nimepewa karama ya kusema lugha aina nyingi mbalimbali kuliko yeyote kati yenu.

19Lakini wakati wa mikutano ya kanisa napenda kuzungumza maneno matano ninayoyaelewa kuliko maelfu ya maneno katika lugha zingine. Ni afadhali nizungumze nikiwa katika uelewa wangu ili niwafundishe wengine.

20Ndugu zangu, msiwaze kama watoto wadogo. Iweni kama watoto wachanga katika mambo maovu, lakini katika kuwaza kwenu muwe kama watu wazima, waliokua.

21Kama Maandiko yanavyosema,[#14:21 Kwa maana ya kawaida, “sheria au torati”, ambapo wakati mwingine inamaanisha Agano la Kale.]

“Kwa kutumia wanaozungumza lugha tofauti

na kutumia midomo ya wageni,

nitazungumza na watu hawa,

hata hivyo, hawatanitii.”

Hivi ndivyo Bwana anasema.

22Na kutokana na hili tunaona kwamba matumizi ya lugha zingine ni ishara kuonesha namna ambavyo Mungu anawashughulikia wasioamini, na si walioamini. Na unabii unaonesha namna ambavyo Mungu hutenda kazi kupitia wanaoamini, na si wasioamini.

23Chukulieni kuwa kanisa lote limekusanyika nanyi nyote mkaanza kusema kwa lugha zingine. Ikiwa baadhi ya watu wasio sehemu ya kundi lenu au wasio waamini wataingia katika kusanyiko lenu, watasema ninyi ni wendawazimu.

24Lakini chukulieni kuwa ninyi nyote mnatabiri na mtu asiyeamini ama asiyekuwa sehemu ya kundi lenu akaingia. Dhambi zao zitawekwa wazi kwao, na watahukumiwa kwa kila kitu mtakachosema.

25Mambo ya siri katika mioyo yao yatajulikana. Na watapiga magoti na kumwabudu Mungu. Watakiri na kusema, “Pasipo shaka, Mungu yuko hapa pamoja nanyi.”[#14:25 Tazama Isa 45:14 na Zek 8:23.]

Mikutano Yenu Inapaswa Kuwasaidia Wote

26Basi ndugu, mnapaswa kufanya nini? Mnapokusanyika, mtu mmoja ana wimbo, mwingine ana mafundisho na mwingine ana kweli mpya kutoka kwa Mungu. Mmoja anasema kwa lugha nyingine na mwingine anafasiri lugha hiyo. Cho chote mnachofanya lazima kiwe na lengo la kumfanya kila mmoja wenu akue katika imani.

27Mnapokusanyika, ikiwa kuna yeyote atasema na kanisa katika lugha, iwe watu wawili tu au isiwe zaidi ya watu watatu. Na wanapaswa wanene kwa zamu, mmoja baada ya mwingine. Na mwingine afasiri kile wanachosema.

28Lakini ikiwa hakuna mfasiri, basi mtu yeyote anayesema kwa lugha nyingine anapaswa kunyamaza kimya. Wanapaswa kuzungumza katika nafsi zao wenyewe ama na Mungu.

29Na manabii wawili au watatu tu ndiyo wanapaswa kuzungumza. Wengine watathmini kile wanachosema.

30Na ujumbe kutoka kwa Mungu ukimjia mtu aliyekaa, mzungumzaji wa kwanza anapaswa kunyamaza.

31Nyote mnaweza kutabiri mmoja baada ya mwingine. Kwa njia hii kila mmoja anaweza kufundishwa na kutiwa moyo.

32Roho za manabii ziko chini ya udhibiti wa manabii wenyewe.[#14:32 Yaani, manabii wanaweza wakajizuia na kusubiri zamu yao kwa utaratibu mzuri.]

33Mungu si Mungu wa machafuko lakini ni Mungu wa amani. Hii ni kanuni kwa ajili ya mikutano yote ya watu wa Mungu.

34Wanawake wanapaswa kunyamaza katika mikutano hii ya kanisa. Kama Sheria ya Musa inavyosema, hawaruhusiwi kuzungumza pasipo utaratibu bali wawe chini ya mamlaka.

35Wakiwa na jambo wanalotaka kujua, wawaulize waume zao nyumbani. Ni aibu kwa mwanamke kuzungumza pasipo utaratibu katika mikutano ya kanisa.

36Je! ni kutoka kwenu neno la Mungu lilikuja ama lilikuja kwa ajili yenu pekee?

37Ikiwa yeyote kati yenu anafikiri kuwa yeye ni nabii au kwamba ana karama ya kiroho, anapaswa kuelewa kuwa ninachowaandikia ninyi nyote ni amri ya Bwana.

38Ikiwa yeyote miongoni mwenu hatalikubali hili, basi hatakubaliwa.

39Hivyo ndugu zangu, mzingatie sana kutabiri. Na msimzuie mtu yeyote kutumia karama ya kusema katika lugha zingine.

40Lakini kila kitu kifanywe kwa usahihi na kwa utaratibu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International