The chat will start when you send the first message.
1Sasa ndugu zangu, ninataka mkumbuke Habari Njema niliyowahubiri. Mliupokea ujumbe huo na endeleeni kuishi kwa kuufuata.
2Habari Njema hiyo, ujumbe mliousikia kutoka kwangu, ni njia ya Mungu kuwaokoa. Ni lazima mwendelee kuuamini. Ikiwa mtaacha, kuamini kwenu ni bure.
3Niliwapa ujumbe nilioupokea. Niliwaambia ukweli muhimu zaidi ya kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema;
4kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema
5na kwamba alimtokea Petro kisha mitume kumi na wawili.
6Baada ya hilo, aliwatokea waamini wengine zaidi ya mia tano kwa wakati mmoja. Wengi wao bado wanaishi sasa, lakini wengine wamekwisha kufa.
7Kisha alimtokea Yakobo na baadaye aliwatokea mitume wote.
8Mwisho wa yote kabisa alinitokea mimi. Nilikuwa tofauti, kama mtoto anayezaliwa wakati usiostahili.
9Mitume wengine wote ni wakuu kuliko mimi. Ninasema hivi kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. Ndiyo sababu sistahili hata kuitwa mtume.
10Lakini, kwa sababu ya neema ya Mungu, ndivyo hivi nilivyo. Na neema aliyonipa haikupotea bure bila manufaa. Nilifanya kazi kwa bidii kuliko mitume wengine wote. (Lakini, kwa hakika si mimi niliyekuwa nafanya kazi. Ni neema ya Mungu iliyo ndani yangu.)
11Hivyo basi, si muhimu ikiwa ni mimi au mitume wengine ndiyo waliowahubiri, sisi sote tunawahubiri watu ujumbe huo huo, na hiki ndicho mlichoamini.
12Tunamwambia kila mtu kuwa Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Hivyo kwa nini baadhi yenu mnasema watu hawatafufuliwa kutoka kwa wafu?
13Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu.
14Na ikiwa Kristo hakufufuliwa, ujumbe tunaowahubiri ni bure. Na imani yenu ni bure.
15Nasi tutakuwa na hatia ya kutoa ushuhuda wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumewahubiri watu kuhusu Yeye, kwa kusema kuwa alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Na ikiwa hakuna anayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Mungu hakumfufua Kristo.
16Ikiwa wale waliokufa hawatafufuliwa, basi Kristo hakufufuliwa pia.
17Na ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, basi imani yenu ni bure; bado mngali watumwa wa dhambi zenu.
18Na watu wa Kristo waliokwisha kufa wamepotea.
19Ikiwa tumaini letu katika Kristo ni kwa ajili tu ya maisha haya hapa duniani, basi watu watuhurumie sisi kuliko mtu mwingine yeyote.
20Lakini hakika Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu; ndiye wa kwanza miongoni mwa wafu wote watakaofufuliwa.
21Kifo huja kwa watu kwa sababu ya tendo la mtu mmoja. Lakini sasa kuna ufufuo kutoka kwa wafu kwa sababu ya mtu mwingine.
22Ndiyo, kwa sababu sisi sote ni wa Adamu, sisi sote tunakufa. Kwa njia hiyo hiyo, sisi sote tulio wa Kristo, tutakuwa hai tena.
23Lakini kila mmoja atafufuliwa kwa mpango sahihi. Kristo alikuwa wa kwanza kufufuliwa. Kisha atakaporudi, wale walio wake watafufuliwa.
24Ndipo mwisho utakuja. Kristo atamwangamiza kila mtawala na kila mamlaka na nguvu. Kisha atampa Mungu Baba ufalme.
25Kristo lazima atawale mpaka Mungu atakapowaweka adui zake wote chini ya udhibiti wake.[#15:25 Kwa maana ya kawaida, “kuweka chini ya miguu”.]
26Adui wa mwisho kuangamizwa ni kifo.
27Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu ameweka kila kitu chini ya udhibiti wake.” Inaposema “kila kitu” kimewekwa chini yake, hii ni wazi Mungu peke yake ndiye ambaye hayuko chini yake. Mungu ndiye anayeweka kila kitu chini ya udhibiti wa Kristo.[#Zab 8:6]
28Baada ya kuweka kila kitu chini ya Kristo, ndipo yeye mwenyewe, kama Mwana, atawekwa chini ya Mungu. Katika namna hii Mungu atakuwa mtawala mkuu juu ya kila kitu.
29Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, sasa watu wanafikiri wanafanya nini kwa kubatizwa kwa ajili ya wale waliokufa? Ikiwa wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini watu wanabatizwa kwa ajili yao?
30Na vipi kuhusu sisi? Kwa nini tunajiweka katika hatari wakati wote?
31Ninakumbana na kifo kila siku. Ni kweli, ndugu zangu kwamba ninajivuna kwa sababu ninyi ni wa Kristo Yesu Bwana wetu.
32Niliwapiga wanyama wa porini kule Efeso. Ikiwa nilifanya hivyo kwa sababu za kibinadamu tu, sijapata kitu. Ikiwa hatufufuliwi kutoka kwa wafu, “basi tule na tunywe, kwa sababu tutakufa kesho.”[#Isa 22:13; 56:12]
33Msidanganywe: “Marafiki wabaya huharibu tabia njema.”
34Rudieni kuwaza kwenu kwa usahihi na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hamumjui Mungu. Ninasema hivi ili niwafedheheshe.
35Lakini mtu mmoja anaweza kuuliza, “Waliokufa wanafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?”
36Haya ni maswali ya kijinga. Unapopanda kitu fulani, ni lazima kife udongoni kabla hakijawa hai na kuota.
37Na unapopanda kitu fulani, unachopanda hakina “mwili” sawa na ule kitakachokuwa nao baadaye. Unapanda mbegu, pengine ngano au kitu kingine.
38Na yeye Mungu hutoa mwili kwa kila aina ya mbegu.
39Vitu vyote vilivyoumbwa kwa mwili haviko sawa: Wanadamu wana aina moja ya mwili, wanyama wana aina nyingine, ndege wana nyingine na samaki nao wana aina yao.
40Pia kuna miili ya kimbingu na miili ya kidunia. Lakini uzuri wa miili ya kimbingu ni wa aina yake na uzuri wa miili ya kidunia ni kitu kingine.
41Jua lina uzuri wa aina yake, mwezi una aina yake na nyota zina aina nyingine ya uzuri. Na kila nyota iko tofauti kwa uzuri wake.
42Ndivyo itakavyokuwa waliokufa watakapofufuliwa na kuwa hai. Mwili “uliopandwa” kaburini utaharibika na kuoza, lakini utafufuliwa katika uhai usioharibika.
43Mwili hauna heshima “unapopandwa”. Lakini utakapofufuliwa, utakuwa na utukufu. Mwili unakuwa dhaifu “unapopandwa”. Lakini unapofufuliwa, unakuwa na nguvu nyingi.
44Mwili unaopandwa ni mwili wa kawaida, wa asili. Utakapofufuliwa utakuwa mwili wa ajabu uliopewa uwezo na Roho.
Kuna mwili wa asili unaoonekana kwa macho. Na hivyo kuna mwili wa Kiroho wa ajabu.
45Kama Maandiko yanavyosema, “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe asili kilichokuwa hai.” Lakini Adamu wa mwisho akafanyika roho.[#15:45 Kwa maana ya kawaida, “nafsi”.; #Mwa 2:7; #15:45 Jina Adamu linamaanisha “mtu”. Inaposema “Adamu wa Mwisho” inamaanisha Kristo, “mtu wa mbinguni”.]
46Mtu wa kiroho hakuja kwanza. Mtu wa asili anayeonekana kwa macho ndiye alikuja kwanza; kisha akaja wa kiroho.
47Mtu wa kwanza alitokana na mavumbi ya dunia. Mtu wa pili alitoka mbinguni.
48Watu wote ni wa dunia. Wako sawa na yule mtu wa kwanza wa dunia. Lakini wale walio wa mbinguni wako kama mtu wa mbinguni.
49Tumeivaa sura ya mtu aliyetoka mavumbini, pia tutaivaa sura ya mtu aliyetoka mbinguni.
50Ninawaambia hili ndugu zangu: Miili yetu na nyama na damu haiwezi kuwa na nafasi katika ufalme wa Mungu. Kitu kitakachoharibika hakiwezi kuwa na sehemu katika kitu kisichoharibika kamwe.
51Lakini sikilizeni, ninawaambia siri hii: Sote hatutakufa, lakini sote tutabadilishwa.
52Itachukuwa sekunde moja. Tutabadilishwa kufumba na kufumbua. Hili litatokea parapanda ya mwisho itakapopulizwa. Parapanda itakapolia wale waliokufa watafufuliwa ili waishi milele. Na tutabadilishwa sote.
53Mungu ataibadilisha miili yetu ili isiharibike kamwe. Mwili huu unaokufa utabadilishwa na kuwa mwili usiokufa.
54Hivyo mwili huu unaokufa utajivika kutokufa. Hili litakapotokea, ndipo Maandiko yatatimilizwa:
“Mauti imemezwa katika ushindi.
55Ewe kifo, ushindi wako uko wapi?
Nguvu yako ya kudhuru iko wapi?”
56Dhambi ni nguvu ya mauti inayodhuru, na nguvu ya dhambi ni sheria.
57Lakini tunamshukuru Mungu anayetupa ushindi kupitia Yesu Kristo Bwana wetu!
58Hivyo, kaka na dada zangu, simameni imara. Msiruhusu kitu chochote kiwabadilishe. Jitoeni nafsi zenu kikamilifu kwa kazi yenu katika Bwana. Mnajua ya kuwa chochote mnachofanya kwa ajili ya Bwana hakitapotea bure bila manufaa.