The chat will start when you send the first message.
1Wapendwa wanangu, ninawaandikieni waraka huu ili kwamba msitende dhambi. Ila kama yeyote akitenda dhambi, tunaye Yesu Kristo wa kutusaidia. Yeye daima alitenda haki, kwa hiyo anaweza kututetea mbele za Mungu Baba.
2Yesu ndiye njia ambapo dhambi zetu zinaondolewa. Naye haziondoi dhambi zetu tu bali anaziondoa dhambi za watu wote.
3Kama tukitii mambo ambayo Mungu ametuamuru kuyafanya, tunapata uhakika ya kuwa tunamjua.
4Kama tukisema kuwa tunamjua Mungu lakini hatuzitii amri zake, tunasema uongo. Kweli haimo ndani mwetu.
5Lakini tunapotii mafundisho ya Mungu, kwa hakika upendo wake unakamilika ndani yetu. Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa tunaishi ndani yake.
6Kama tukisema kuwa tunaishi ndani ya Mungu, ni lazima tuishi kwa namna ambvyo Yesu aliishi.
7Wapendwa rafiki zangu, siwaandiki ninyi amri mpya. Ni amri ile ile ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ni fundisho lile lile ambalo mmekwishalisikia.
8Lakini kile ninachokiandika pia ni amri mpya. Ni kweli; Mnaweza kuiona kweli ndani ya Yesu na ndani yenu ninyi wenyewe. Giza linatoweka, na nuru ya kweli tayari inang'aa.
9Mtu anaweza kusema, “Niko nuruni,” lakini ikiwa anamchukia ndugu yeyote katika familia ya Mungu, basi angali bado katika giza.
10Wao wanaowapenda ndugu wanaishi katika nuru, na hakuna kitu ndani yao cha kuwafanya watende mabaya.
11Lakini yeyote anayemchukia nduguye wa kike au wa kiume yuko gizani. Anaishi katika giza. Hajui anakoenda, kwa sababu giza limemfanya asiweze kuona.
12Ninawaandikia, ninyi watoto wapendwa,
kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa njia ya Kristo.
13Ninawaandikia, ninyi akina baba,
kwa sababu mnamjua yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia, ninyi vijana,
kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
14Ninawaandikia ninyi watoto,
kwa sababu mnamjua Baba.
Ninawaandikia ninyi, akina baba,
kwa sababu mnamfahamu yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia ninyi, vijana,
kwa sababu mna nguvu.
Mafundisho ya Neno la Mungu yimo ndani yenu,
na mmemshinda yule mwovu.
15Msiipende dunia hii ya uovu wala mambo yaliyomo ndani yake. Kama mkiipenda dunia, upendo wa baba haumo ndani yenu.
16Yote yaliyomo katika dunia: yaani, tamaa halisi za kibinadamu, tamaa kwa yale mabaya tunayoyaona, na kiburi cha vitu tulivyonavyo. Lakini hakuna hata mojawapo ya haya litokalo kwa Baba. Yote yanatoka katika dunia.
17Dunia inapita, na mambo yote ambayo watu wanayataka kutoka katika dunia nayo yanapita. Lakini yeyote atendaye mambo ambayo Mungu anayataka ataishi milele.
18Wapendwa wanangu, mwisho umekaribia! Mmesikia kuwa adui wa Kristo anakuja. Na sasa maadui wengi wa Kristo tayari wapo hapa. Hivyo tunajua kwamba mwisho umekaribia.
19Maadui hawa walikuwa miongoni mwetu, lakini walituacha. Hawakuwa wenzetu hasa. Kama wangelikuwa kweli wenzetu, wangebaki pamoja nasi. Lakini walituacha. Hii inaonesha kuwa hakuna hata mmoja wao aliyekuwa kwa hakika mwenzetu.
20Mnayo karama aliyowapa Yeye Aliye Mtakatifu. Hivyo nyote mnaijua kweli.[#2:20 Kwa maana ya kawaida, “upako”. Hili linaweza kumaanisha Roho Mtakatifu. Au Mafundisho au Kweli kama ilivyo katika mstari wa 24. Pia katika mstari wa 27.; #2:20 Mungu au Kristo.]
21Mnadhani ninawaandikia waraka huu kwa sababu hamuijui kweli? Hapana! Ninawaandikia kwa sababu mnaijua kweli. Na mnajua kuwa hakuna uongo utokao katika kweli.
22Ni nani basi aliye mwongo? Ni yeye anayesema kuwa Yesu siyo Kristo. Yeyote anayesema hivyo ni adui wa Kristo. Yeye huyo asiyemwamini Baba wala Mwana.
23Yeyote asiyemwamini Mwana hana Baba, ila yeye anayemkubali Mwana anaye Baba pia.
24Mnapaswa kuendelea kuyafuata mafundisho mliyoyasikia tangu mwanzo. Kama mkifanya hivyo, mtakuwa siku zote katika Mwana na katika Baba.
25Na hili ndilo ambalo Mwana ameliahidi kwetu sisi, uzima wa milele.
26Ninawaandikia barua hii juu ya wale ambao wanataka kuwapotosha katika njia isiyo sahihi.
27Kristo aliwapa karama maalumu. Nanyi bado mngali na karama hiyo ndani yenu. Hivyo hamumhitaji yeyote kuwafundisha. Karama aliyowapa inawafundisha juu ya kila jambo. Ni karama ya kweli, si ya uongo. Hivyo endeleeni kuishi katika Kristo, kama karama yake ilivyowafundisha.[#2:27 Kwa ufasaha “upako”.]
28Ndiyo, wanangu wapendwa, ishini ndani yake. Kama tukifanya hivyo, hatutakuwa na hofu siku kristo atakapo kuja tena. Hatutahitaji kujificha na kuwa na aibu ajapo.
29Mnajua ya kwamba daima Kristo alifanya yaliyo ya haki. Vivyo hivyo mnajua pia ya kwamba wote watendao haki ni watoto wa Mungu.