1 Yohana 4

1 Yohana 4

Yohana Aonya juu ya Walimu wa Uongo

1Rafiki zangu wapenzi, manabii wengi wa uongo wapo duniani sasa. Hivyo msiiamini kila roho, lakini zijaribuni hizo roho ili muone kama zinatoka kwa Mungu.

2Hivi ndivyo mwezavyo kuitambua Roho ya Mungu. Roho inayosema, “Naamini kuwa Yesu ni Masihi aliye kuja duniani na akafanyika mwanadamu.” Roho hiyo inatoka kwa Mungu.

3Roho inayokataa kutamka hayo juu ya Yesu, hii ni roho iliyo adui kwa Kristo. Mmesikia kuwa adui wa kristo anakuja, na sasa amekwishakuja naye yupo tayari ulimwenguni.

4Wanangu wapenzi, ninyi ni wa Mungu, hivyo mmeshawashinda tayari hawa manabii wa uongo. Hii ni kwa sababu yule aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliyeko duniani.

5Wao ni wa ulimwengu. Hivyo kile wanachokisema ni cha ulimwengu pia. Na ulimwengu husikia kile wanachokisema.

6Lakini sisi tunatokana na Mungu. Kwa hiyo watu wanaomjua Mungu hutusikia sisi. Lakini watu wasiotokana na Mungu hawatusikii sisi. Hivi ndivyo tunavyiojua Roho iliyo ya kweli na ile iliyo ya uongo.

Upendo Hutoka kwa Mungu

7Wapenzi rafiki, tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi, kwa sababu upendo watoka kwa Mungu. Yeyote apendae amefanyika mwana wa Mungu. Na kila apendae anamfahamu Mungu.

8Kila asiyependa hamfahamu Mungu, kwa sababu Mungu ni Pendo.

9Hivi ndivyo Mungu alivyo tuonyesha pendo lake sisi: Alimtuma mwanawe wa pekee ulimwenguni kutupatia sisi uzima katika yeye.

10Upendo wa kweli ni upendo wa Mungu kwa ajili yetu, si upendo wetu kwa Mungu. Alimtuma mwanawe kama njia ya kuziondoa dhambi zetu.

11Hivyo ndivyo Mungu atupendavyo, rafiki wapenzi! Kwa hiyo tupendane sisi kwa sisi.

12Hakuna aliyemwona Mungu. Ila tukipendana sisi kwa sisi, Mungu anaishi ndani yetu. Kama tukipendana sisi kwa sisi, Upendo wa Mungu unafikia shabaha yake na unafanywa kamili ndani yetu.

13Twatambua kuwa tunaishi katika Mungu na mungu ndani yetu. Twalitambua hilo kwa sababu ametupa Roho wake.

14Tumeona kuwa Baba alimtuma mwanaye aje kuwa Mwokozi wa ulimwengu, na hili ndilo tunalowaambia watu sasa.

15Yeyote anayesema, “Naamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu,” huyo ni mtu anayeishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani ya mtu huyo.

16Hivyo twalifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu, na tunalitumainia pendo hilo.

Mungu ni pendo. Kila anae ishi katika pendo anaishi ndani ya Mungu, na Mungu ndani yao.

17Kama pendo la Mungu limekamilishwa ndani yetu, tunaweza kuwa bila hofu siku ambayo Mungu atahukumu ulimwengu. Hatutakuwa na hofu, kwa sababu katika ulimwengu huu tunaishi kama Yesu.[#4:17 Kwa maana ya kawaida, “Yeye Yule”.]

18Palipo na upendo wa Mungu, hakuna hofu, kwa sababu upendo wa Mungu ulio kamili unaondoa hofu. Ni hukumu yake ndiyo inayomfanya mtu kuwa na hofu. Hivyo pendo lake halikamilishwi kwa mtu ambaye ndani yake kuna hofu.

19Tunapenda kwa sababu Mungu alitupenda sisi kwanza.

20Kama tukisema kuwa tunampenda Mungu na tunamchukia mmojawapo wa kaka na dada zetu katika familia ya Mungu, basi sisi tu waongo. Kama hatuwezi kumpenda mtu tunayemwona, tutawezaje kumpenda Mungu, ambaye hata hatujamwona.

21Mungu ametupa amri hii: Kama tunampenda Mungu, Ni lazima pia tupendane sisi kwa sisi kama kina kaka na kina dada.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International