The chat will start when you send the first message.
1Vivyo hivyo, enyi wake mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu. Ili hata wale waliokataa kuyapokea mafundisho ya Mungu washawishike na kuamini kutokana na jinsi mnavyoishi. Hivyo hamtahitaji kusema chochote.
2Waume zenu watayaona maisha safi mnayoishi yanayomheshimu Mungu.
3Si nywele za gharama, vito vya dhahabu, au nguo nzuri zitakazowafanya mpendeze.
4Bali, uzuri wenu utoke ndani yenu, uzuri wa roho yenye upole na utulivu. Uzuri huo hautatoweka kamwe. Ni wa thamani sana kwa Mungu.
5Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanawake watakatifu walioishi hapo zamani na kumfuata Mungu. Walijipamba kwa jinsi hiyo hiyo kwa kuwahudumia waume zao.
6Ninazungumza juu ya wanawake kama Sara aliyemtii Abrahamu, mume wake na kumwita bwana wake. Na ninyi wanawake ni watoto wa kweli wa Sara ikiwa daima mnafanya yale yaliyo sahihi pasipokuwa na hofu.
7Vivyo hivyo, enyi waume inawapasa kuishi na wake zenu kwa kuelewa udhaifu alionao mwanamke na matumaini ya Mkristo. Hamna budi kuwapa heshima kwa sababu Mungu kwa sababu Mungu anawapa baraka zile zile anazowapa ninyi, yaani neema ya maisha ya kweli. Fanyeni hivi ili maombi yenu yasizuiliwe.
8Hivyo ninyi nyote mnapaswa kuishi pamoja kwa amani. Mjitahidi kuelewana ninyi wenyewe. Mpendane kama kaka na dada na muwe wanyenyekevu na wema.
9Msimfanyie uovu mtu yeyote ili kulipa kisasi kwa uovu aliowatendea. Msimtukane mtu yeyote ili kulipiza matusi aliyowatukana. Lakini mwombeni Mungu awabariki watu hao. Fanyeni hivyo kwa sababu ninyi wenyewe mliteuliwa kupokea baraka,
10Maandiko yanasema:
“Anayetaka kufurahia maisha ya kweli
na kuwa na siku nyingi njema tu,
aepuke kusema chochote kinachoumiza,
na asiruhusu uongo utoke kwenye kinywa yake.
11Aache kutenda uovu, na atende mema.
Atafute amani, na fanya kila analoweza ili kuwasaidia watu kuishi kwa amani.
12Bwana huwaangalia wale watendao haki,
na husikia maombi yao.
Lakini yu kinyume cha wale watendao uovu.”
13Ikiwa unajaribu kwa bidii kutenda mema, ni nani atakayetaka kukudhuru?
14Lakini hata ukiteseka kwa sababu kutenda yaliyo haki, unazo Baraka za Mungu. “Msimwogope mtu yeyote, wala msiruhusu watu wawasumbue.”[#Isa 8:12]
15Lakini mjitoe kikamilifu kwa Kristo ambaye ni Bwana wenu pekee. Na daima iweni tayari kumjibu mtu yeyote anayetaka ufafanuzi kuhusu tumaini linaloyaongoza maisha yenu.[#3:15 Kwa maana ya kawaida, “tumaini lililo ndani (au miongoni) mwenu,” Hii inamaana kuwa, “kile kinachothibiti tabia zenu kama waamini.”]
16Lakini wajibuni kwa upole na heshima kwa ajili ya Mungu, mkizitunza dhamiri zenu mbele zake. Ndipo watu watakapoona namna njema mnayoishi kama wafuasi wa Kristo. Na wataaibika kwa kuwanenea mabaya.
17Ni afadhali kuteseka kwa kutenda mema kuliko kutenda mabaya. Ndiyo, ni bora ikiwa hivyo ndivyo Mungu anavyotaka.
18Kristo mwenyewe aliteseka alipokufa kwa ajili yenu,
na kwa kifo hicho kimoja alilipa fidia kwa ajili ya dhambi.
Hakuwa na hatia,
lakini alikufa kwa ajili ya watu waliokuwa na hatia.
Alifanya hivyo ili awalete ninyi nyote kwa Mungu.
Kama mwanadamu, aliuawa,
lakini uhai wake ulifanywa hai na Roho.
19Na kwa Roho alikwenda akazihubiri roho zilizo kifungoni.
20Hizo ndizo roho zilizokataa kumtii Mungu hapo zamani wakati wa Nuhu. Mungu alisubiri kwa uvumilivu Nuhu alipokuwa anaunda safina. Na watu wachache tu, yaani wanane kwa jumla ndiyo walioingia katika safina na kuokolewa kwa kuvushwa salama katika gharika hiyo.
21Na maji yale ni kama ubatizo, unaowaokoa ninyi sasa kupitia ufufuo wa Yesu Kristo kutoka katika wafu na siyo kuondoa uchafu mwilini kwa kuoga. Ni ahadi ya dhati ya kuishi kwa kumcha Mungu.
22Sasa yupo mbinguni upande wa kuume wa Mungu, na anatawala juu ya malaika, mamlaka na nguvu.